The House of Favourite Newspapers

CCM Vs Chadema, Huku Mangula Kule Lowassa, Hapatoshi Monduli

BAADA ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Monduli mkoani Arusha, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula ataongoza jahazi kuzindua kampeni za uchaguzi za chama hicho huku upande wa Chadema ukiongozwa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, na Mbunge wa Monduli kipindi hicho, Edward Lowassa, Jumatano Agosti 29, 2018 .
Katika uchaguzi huo utakaofanyika Septemba 16, Mangula atazindua kampeni za CCM Monduli Mjini 
ambapo Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa Arusha, Shaaban Mdoe amesema tayari maandalizi ya uzinduzi wa kampeni yamekamilika.
Aidha, Mgombea Ubunge wa CCM, Julius Kalanga amesema amejiandaa na wana CCM kutetea jimbo hilo ambalo alijiuzulu akiwa mbunge wa Chadema ambapo katika uchaguzi huo, vyama vinane vinashiriki.
Kwa upande wa Chadema, Edward Lowassa ambaye pia in Mjumbe wa Kamati kuu Chadema, atazindua kampeni za uchaguzi mdogo wa Monduli katika eneo la Mtowambu siku hiyo hiyo.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa amesema wamejipanga Jumatano Agosti 29 kuzindua kampeni kwa kishindo na kusema chama hicho kinajua michezo michafu ambayo inaendelea kufanywa na CCM, lakini wanataka dunia ijue CCM haikubaliki tena.
Chadema wamempitisha kugombea diwani wa Lepurko, Yonas Laizer. Kata hiyo ndiyo anakotoka Kalanga ambaye pia alikuwa diwani wa kata hiyo hadi mwaka 2015 akiwa CCM na kujiunga na Chadema.
Wagombea wengine katika jimbo hilo ni Omar Kawanga (DP), Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini), Fransis Ringo (Aada-Tadea), Elizabeth Salewa (AAFP) na Wilfred Mlay (ACT-Wazalendo).

Comments are closed.