Waziri Mchengerwa atangaza matokeo ya jumla Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 – Video
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ametangaza matokeo ya jumla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchini Novemba 27,2024.
Matokeo hayo ameyatangaza usiku wa Novemba 28,2024 jijini Dodoma ambapo amesema katika uchaguzi huo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi wa jumla wa wenyeviti wa serikali za vijiji kwa nafasi ya viti 12,150 sawa na asilimia 99.01.
Aidha,Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata jumla ya viti 97 sawa na asilimia 0.79 ya matokeo ya uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, Mchengerwa amesema kuwa,itongoji nane wagombea wake walifariki dunia hivyo uchaguzi utarudiwa na 37 havikufanya uchaguzi Novemba 27, 2024.
Waziri Mchengerwa amesema,kati ya hivyo, vitongoji havikufanya uchaguzi kwa kuwa wagombea wake walifariki baada ya zoezi la uteuzi.
Amesema,wagombea hao walitoka katika Halmashauri za wilaya za Kilwa (2), Nanyumbu (1), Itilima (1), Ikungi (1), Manyoni (1), Uyui (1) na Mbarali.
Waziri Mchengerwa amesema, vitongoji 29 havikufanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali. Katika mtaa mmoja wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga hakupatikana mshindi kwa sababu kura za wagombea wawili zilifungana.
Aidha, vitongoji 12 vitarudia uchaguzi kwa kuwa matokeo ya wagombea yalifungana na vitongoji tisa vitarudia uchaguzi kutokana na wagombea pekee kutopata kura za kutosheleza
Waziri Mchengerwa amesema,Chama cha ACT kimepata viti 11 sawa na asilimia 0.09, Chama cha CUF kimepata jumla ya viti 10 sawa na asilimia 0.08, NCCR Mageuzi kimepata kiti kimoja sawa na asilimia 0.01.
Waziri Mchengerwa amesema, katika nafasi za Mwenyekiti wa Kitongoji CCM imeshinda nafasi 62,728 sawa na asilimia 98.26, CHADEMA imeshinda nafasi 853 sawa na asilimia 1.34.
ACT Wazalendo imeshinda nafasi 150 sawa na asilimia 0.23, CUF imeshinda nafasi 78 sawa na asilimia 0.12, NCCR -Mageuzi imeshinda nafasi 10 sawa na asilimia 0.02.
Pia,UDP imeshinda nafasi 6 sawa na asilimia 0.01, UMD imeshinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.003 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.002.
Waziri Mchengerwa amesema, CCM kimeshinda viti 4213 sawa na asilimia 98.83 kwenye nafasi za Mwenyekiti wa Mtaa huku CHADEMA imeshinda nafasi 36 sawa na asilimia 0.84.
Kwa upande wa ACT Wazalendo imeshinda nafasi 9 sawa na asilimia 0.21, CUF imeshinda nafasi 4 sawa na asilimia 0.09 na CHAUMA imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.02.