CDC: Kiwango cha Upimaji Corona Marekani Hakitoshi
DKT. Tom Frieden, mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa nchini Marekani (Centers for Disease Control and Prevention) amesema Marekani haipimi kikamilifu watu wanaofanyiwa majaribio ya kugundua iwapo wameambukizwa na virusi vya corona.
Amesisitiza pia kwamba hilo ni jukumu la serikali ya shirikisho.
Wakati wa kuibuka kwa janga la ugonjwa huo, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema mtu yeyote aliyetaka kupimwa angepimwa, hata hivyo, kwa mujibu wa Frieden, magavana kadhaa wamelalamika kwamba hawapati vifaa na madawa ya tiba kiasi cha kutosha.
Amegusia pia kwamba mpango wa Trump wa kufungua mipaka ya nchi hiyo haujumuishi mkakati wa kitaifa wa kufanya upimaji, na amelisukumia jukumu hilo kwa majimbo.
Frieden ambaye ni mtaalam wa magonjwa ya kuambukiza, amesema kiwango cha majaribio ya vipimo kwa watu 150,000 kwa siku hakitoshi.


