Chadema: INEC Haina Mamlaka ya Kuiondoa Kwenye Uchaguzi – Video

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Aprili 15, 2025 kimepinga vikali kauli ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwamba vyama vya siasa vitakavyoshindwa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi vitazuiwa kushiriki uchaguzi ujao.
Mkuu wa Idara ya Sheria wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amesema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba, akibainisha kuwa INEC haina mamlaka ya kisheria ya kuondoa chama au mgombea yeyote kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.
Chadema pia imeeleza kuwa kanuni mpya zinazotajwa na INEC bado hazijaanza kutumika, na ratiba ya kisheria hairuhusu utekelezaji wake hadi siku moja kabla ya uteuzi rasmi wa wagombea — hali ambayo haiwezekani bila Bunge kusitishwa, jambo linalotarajiwa kutokea mwishoni mwa Juni.