The House of Favourite Newspapers

Chadema Kwenda na Majeruhi wa Risasi Mahakamani

UPANDE utetezi kwenye kesi ya uchochezi namba 112/2018, inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, leo Septemba 24, 2019 umesema umepanga kwenda mahakamani na mashahidi waliojeruhiwa kwa risasi huku wakiomba ahirisho la kesi hiyo, kutokana na washtakiwa wawili kutokuwepo huku hoja nyingine ikiwa ni kijipanga kwa ushahidi.

 

Katika kesi hiyo, iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Dk. Vincent Mashinji, hakuwepo mahakamani kutokana na dharura.

Dk. Mashinji na Ester Matiko ambao ni miongoni mwa washtakiwa hao, kupitia wakili wao Prof. Abdallah Safari, wameomba ruhusa ya mahakama kusafiri nje nchi.

 

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa; Dk. Mashinji, Katibu Mkuu wa chama hiko; John Mnyika, Naibu Katibu Bara na Salum Mwalimu, Naibu Katibu Zanzibar.

Wengine ni Halima Mdee, Mbunge wa Kawe; Matiko ambaye ni Mbunge wa Tarime Mjini; Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini; John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini na Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini.

 

Mbali na Prof. Safari, upande wa utetezi umewakilishwa na Peter Kibatala, Hekima Mwasipu, John Mallya na Dickson Matata.

Upande wa serikali umewakilishwa na Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mchimbi,Wakili wa Serikali Mkuu; Wankyo Simon, Wakili wa Serikali Mwandamizi.

 

Awali, Profesa Safari amedai, kuwa mshtakiwa Dk. Mashinji amehudhuria kwenye kesi namba 9 ya mwaka 2017 ya uchochezi inayomkabili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea ambayo ilikuwa kwenye hatua ya ukilizwaji.

Amedai, upande wa Jamhuri haukuweka wazi idadi ya mashahidi wala siku yao ya kufunga ushahidi wao, na waliushtukiza upande wa utetezi ilhali wanajua kuna maandalizi ya utetezi.

Prof. Safari ameitaja ibara ya 13 ya Katiba inayoeleza juu ya haki ya kusikilizwa kwa washtakiwa kikamilifu.

 

Licha ya kuieleza mahakama hiyo kuwa tarehe 26 Septemba hadi tarehe 6 Oktoba 2019, mshtakiwa Mashinji ameiandikia barua kuwa atakuwa safarini Uengereza, upande huo wanao mashahidi waliojeruhiwa kwa risasi ambao wanawaanda kuwaleta mahakamani hapo.

 

Prof. Safari amedai mahakamani hapo, mshitakiwa  wa tano (Matiko), amealikwa kupitia Ofisi ya Bunge kuanzia tarehe 25 hadi 28 Septemba mwaka huu kwenda Kigali-Rwanda.

Hata Prof. Safari ameeleza kuwa 13 – 18, Oktoba 2019, mshtakiwa Matiko amealikwa kwenye Bunge la Umoja wa Ulaya kama Mjumbe wa Afrika. Baada ya kueleza hayo, Prof. Safari ameiomba mahakama kupanga siku ya tarehe 7 na 8 Oktoba mwaka huu kwa ajili ya kuendelea.

 

Wakili Nchimbi akijibu hoja hizo, ameeleza kwa kuwa wito wa Dk. Mashinji mahakamani unaonekana aliitwa kwenye kesi jana, hivyo leo anaweza kuwa njiani na kesho akaja mahakamani kwa ajili ya kuendelea.

 

Nchimbi ameeleza, kuwa katika barua ya kuomba mahakama ruhusa ya safari ya Dk. Mashinji, haikuainisha anakwenda Uengereza kufanya nini.

 

Pia Nchimbi ameeleza, dharura ya Matiko ya kwenda Kigali, Rwanda ni ombi linalotoka kwenye Taasisi ya Mawakili Wanawake wa Tanzania (TAWLA), lilowasilishwa kwa katibu wa wabunge, hivyo anaweza kukubaliwa ama kukataliwa na kwamba, wapo wabunge sita, yeye hana ulazima wa kwenda.

 

Baada ya kusiliza pande zote mbili, Hakimu Simba ameamua kuahirisha shauri hilo mpaka kesho tarehe 25  atakapotoa uamuzi juu ya mabishano hayo.

Comments are closed.