The House of Favourite Newspapers

Chadema Yapinga Kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, Mnyika Afunguka!

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Ndugu John Mnyika ameufahamisha umma kwamba hatohudhuria na hatoshiriki kwenye kikao cha leo Aprili 12, 2025 kilichoitishwa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi kikihusisha vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki kwenye uchaguzi Mkuu ujao kwaajili ya kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Kulingana na Taratibu, wawakilishi wa vyama vya siasa katika Kikao hicho wanatakiwa kuwa Watendaji wakuu wa Vyama (Makatibu wa vyama), kwakuwa ndio wenye mamlaka ya kusaini maadili hayo ya uchaguzi mkuu.

“Katibu Mkuu sijateua kiongozi ama afisa yeyote kwenda kushiriki kwa niaba yangu katika kikao hicho kitakachofanyika kwenye Ofisi za Tume ya Taifa ya uchaguzi Mkoani Dodoma.”imesomeka taarifa ya John Mnyika.

Wakati hayo yanafanyika ikumbukwe kuwa Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ametiwa korokoroni, wakati ambapo Makamu wake mwenyekiti John Heche kupitia kurasa yake ya x amechapisha taarifa akieleza malalamiko yake kadhaa ya kutokuwa na imani na tume hiyo na kile ambacho wametangaza kukifanya hii leo.

“Tume ya Taifa ya uchaguzi nchi hii haijawahi kuwa na maadili, ni tume ambayo inakisaidia Chama Cha Mapinduzi, haiwezi kuwaambia watu wasaini maadili, kwasasa hoja ni moja tu No Reforms, No election”, amesema.