Chadema Yataja Sababu ya Kukataa Kusaini Maadili ya Uchaguzi wa Mwaka 2025
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mawasiliano Bi. Brenda Rupia ameeleza kuwa msimamo wa Chadema kutoshiriki kikao cha Aprili 12, 2025 dhidi ya Vyama vya siasa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi kwaajili ya kusaini maadili ya uchaguzi wa mwaka 2025, mbali ya sababu nyingine, unatokana pia na kupuuzwa kwa kutopewa majibu ya maandishi kuhusu barua yao rasmi iliyowasilishwa na Katibu Mkuu Disemba 29, 2024, akieleza mapendekezo na madai ya msingi ya Chadema kuhusu mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
“Ukimya wa Tume ya Taifa ya uchaguzi unathibitisha kukosekana kwa nia ya dhati ya kufanya mashauriano ya kweli na ya wazi kuhusu mchakato wa uchaguzi.” Imesema taarifa iliyosainiwa na Brenda Rupia.
Aprili 12, 2025 kulingana na Chapisho la Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika kupitia ukurasa wake wa X, amewaambia wananchi na wanachama wa Chadema kuwa hatoshiriki kikao cha kutia saini maadili ya uchaguzi mama kilivyoitishwa na Tume ya Uchaguzi na hajamuidhinisha yeyote kumuwakilisha, wakisisitiza kuwa tayari walishafanya maamuzi yanayojulikana kama No reforms, No election, wakimaanisha kuwa hakuna uchaguzi nchini Tanzania mwaka huu ikiwa hakutakuwepo na mabadiliko ya sheria na mifumo ya kiuchaguzi.
Kulingana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi, Makatibu wakuu wa vyama ndiyo wenye dhamana ya kusaini maadili hayo ya uchaguzi na chama ambacho hakitashiriki katika kikao hicho cha siku moja kitakuwa kimejiondoa rasmi kwenye kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa baadae mwaka huu.