The House of Favourite Newspapers

Chama Akabidhiwa AS Vita

0

CLATOUS Chama, kiungo mshambuliaji wa kikosi cha Simba, amekabidhiwa mchezo dhidi ya AS Vita kuipa ushindi timu hiyo na kutinga robo fainali.

 

Chama mwenye pasi mbili za mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi baada ya kucheza mechi nne, alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoshinda 2-1 dhidi ya AS Vita msimu wa 2018/19, Uwanja wa Mkapa, Dar.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Seleman Matola, Kocha Msaidizi wa Simba, alisema kitakachowapa jeuri ya ushindi kwenye mchezo huo ni uwepo wa wachezaji waliocheza na AS Vita wakiongozwa na Chama kipindi kile wanawaondosha hatua kama hii.

“Tuna mechi ngumu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwemo dhidi ya AS Vita, ila katika hilo hatuna mashaka makubwa kwani tuna wachezaji ambao walicheza dhidi ya AS Vita wakati ule akiwemo Chama na wana uwezo mkubwa wa kutupatia ushindi.

 

“Uwepo wa wachezaji waliocheza hatua za makundi msimu wa 2018/19 ni ushindi kwetu kwani wanajua mbinu ambazo walitumia kupata ushindi, kikubwa mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” alisema Matola.

 

Simba na AS Vita, zitapambana Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni mchezo wa Kund A. Mechi ya kwanza kule DR Congo, Simba ilishinda 1-0 kwa bao la Chris Mugalu.

 

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi, huku wakitamba kuwa wanazitaka pointi tatu.Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema: “Wachezaji ambao hawajajumuishwa katika vikosi vya timu za taifa, wanaendelea na mazoezi kila siku chini ya Kocha Mkuu, Didier Gomes.

 

“Tunajua ugumu na umuhimu wa kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huu, mpaka sasa hakuna mchezaji yeyote aliye na majeraha, hivyo tunachosubiri ni kurejea kwa sehemu ya wachezaji wetu walio kwenye timu zao ili kocha afanye maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo huo.”

Leave A Reply