SIMBA tayari imefanikiwa kuwamaliza wapinzani wao Nkana FC nje ya uwanja na kilichobaki ni ndani ya uwanja, hiyo ni baada ya kufanikiwa kupangua fitna zao zote walizozipanga kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kesho Jumamosi.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kutafuta nafasi ya kucheza Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mchezo ukitarajiwa kupigwa mjini Kitwe, Lusaka nchini Zambia.
Simba ilifika hatua hiyo baada ya kuiondoa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa jumla ya mabao 8-1, wakati Nkana iliiondoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Swedy Mkwabi ambaye ameongozana na timu hiyo, alisema wanashukuru timu imefika salama Zambia na kupata mapokezi mazuri kutoka kwa wenyeji wao ambao ni Klabu ya Power Dynamos aliyokuwa anaichezea kiungo wao, Clatous Chama.
Mkwabi alisema mapokezi hayo waliyapata tangu walipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Southdowns na kupokelewa na viongozi wa Power Dynamos kisha kuwapeleka hotelini walipofikia.
Aliongeza kuwa, baada ya mapokezi hayo jioni walikwenda kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Dynamos ambao walipewa na wenyeji wao hao wanaoutumia huku kukiwa na ulinzi mkali wa askari.
“Kilichobakia hivi sasa ni sisi wenyewe tushindwe kupata matokeo mazuri ugenini, lakini kuhusu fitna zilizokuwa zimepangwa tumejitahidi kuzikwepa kutokana na maandalizi tuliyoyaweka ya kuwatanguliza baadhi ya viongozi wetu.
“Viongozi hao baada ya kufika huko waliandaa mapokezi mazuri kwa maana ya hoteli na kutuandalia uwanja mzuri wa kufanyia mazoezi tuliyofanya jana (juzi Jumatano) na kesho (leo Ijumaa) huku tukipewa mlinzi mzuri na wenyeji wetu timu ya Power Dynamos.
“Pia, tunawashukuru Watanzania waishio hapa nchini Zambia ambao ni mashabiki wa Simba wamekuwa wakitupa ushirikiano mzuri kiukweli, hivyo kilichobaki hivi sasa ni kuwasubiri wapinzani wetu tutakapokutana uwanjani baada ya kufanikiwa kuzikwepa fitna,” alisema Mkwabi.
Katika msafara huo wa Simba uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Simba (C.E.O), Crescentius Magori pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba Haji Manara.
Stori: Ibrahim Mussa, Kitwe na Sweetbert Lukonge, Dar
Comments are closed.