The House of Favourite Newspapers

Chama Anatisha

0

UNAWEZA kusema Clatous Chota Chama anaendelea pale alipoishia kutokana na yale anayoyafanya ndani ya uwanja akiwa na jezi ya Simba SC yenye namba 17 mgongoni.

 

Kiungo huyo raia wa Zambia, amejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo msimu huu uliofungwa Januari 15, mwaka huu akitokea RS Berkane ya Morocco.

 

Chama msimu uliopita, aliachana na Simba aliyoitumikia kwa misimu mitatu na kutimkia RS Berkane, lakini hakudumu sana, akarejea Msimbazi.

 

Tangu arudi Simba, nyota huyo amekuwa na kiwango bora kama ilivyokuwa awali ambapo juzi Ijumaa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, aliendeleza makali yake kwa kufunga bao moja akiwatesa vibaya mabeki.

 

Bao hilo alilifunga dakika ya 18 akipokea pasi ya Pape Ousmane Sakho ambapo kabla ya kufunga, aliwapiga chenga mabeki wawili wa Biashara United, nahodha Abdulmajid Mangalo na Boniface Maganga, kisha akaukwamisha mpira kimiani uliowapita kipa James Ssetuba na beki wake, Fredy Sululu. Simba ilishinda 3-0.

 

Akizungumzia mateso aliyoyapata wakati anamkaba Chama asifunge bao hilo, Mangalo aliliambia Spoti Xtra kwamba: “Unajua kabla mpira haujamfikia Chama, sisi mabeki tulijua Sakho atafunga mwenyewe kutokana na nafasi aliyokuwepo, hivyo tulikuwa katika harakati za kumuwahi kwa nguvu.

 

“Sasa alipopiga pasi kwa Chama, ikatulazimu tubadilishe uelekeo, jambo ambalo lilikuwa gumu sana na kujikuta tunateleza na kuanguka.

 

“Kwa kuwa wajibu mkubwa wa beki ni kuzuia mpira usiingie nyavuni, basi niliamua kuubwaga mwili chini ili ikitokea amepiga mpira niuzuie, lakini tofauti na matarajio yangu, Chama alikuwa na utulivu mkubwa, akausogeza mpira pembeni zaidi na kufunga, nadhani anastahili kupongezwa kwa hilo.

 

“Kwa utulivu aliouonesha akiwa eneo lile na kufunga bao, inaonesha ni mchezaji tishio.”

Mara baada ya mchezo huo, Chama ambaye ana mabao mawili katika Ligi Kuu Bara msimu huu, alisema: “Ni ushindi mwingine muhimu leo (juzi), nina furaha kufunga tena.”

 

Chama tangu arejee Simba, amefanikiwa kufunga mabao sita na asisti tatu katika michuano yote, huku akiwa na hat trick moja aliyopiga katika Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) wakati Simba ikishinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Mkapa, Februari 16, 2022.

STORI: JOEL THOMAS

Leave A Reply