CHAMA tawala Botswana Kimeshindwa katika Uchaguzi wa Wabunge

CHAMA tawala cha Botswana, Botswana Democratic Party (BDP) kimeshindwa katika uchaguzi baada ya kuliongoza taifa hilo kwa takriban miaka 58, tangu mwaka 1966.
Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi amekubali kushindwa baada ya matokeo ya awali kuonesha kuwa vyama vya upinzani vimeshinda takriban viti 35 kati ya 61 bungeni, huku chama tawala kikishinda kiti moja pekee kufikia leo asubuhi.
Chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC), kinachoongozwa na wakili wa haki za binadamu Duma Boko, kilishinda viti 20, kulingana na hesabu za awali.
UDC kinaonekana kitaunda serikali huku kikitarajiwa kupitisha kizingiti cha viti 31 kwa wingi wa wabunge.
Wabunge wanapomchagua rais nchini Botswana, Duma Boko yuko mbioni kuwa mkuu wa nchi mara tu bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza.
Boko, ambaye anagombea kwa mara ya tatu, amewataka wafuasi wake kudumisha umakini na nidhamu.
Licha ya kusimamia mabadiliko makubwa nchini Botswana, ukuaji duni wa uchumi wa hivi karibuni na ukosefu mkubwa wa ajira ulidhoofisha umaarufu wa BDP.
Atachukua nafasi ya Mokgweetsi Masisi ambaye aliingia madarakani tangu 2018 na kuongoza kampeni ya BDP iliyoshindwa kupata matokeo mazuri ya kura.