GAZETI namba moja la Michezo nchini Tanzania, la Championi kupitia kampeni yake ya Tuko Pamoja, leo Jumanne, Oktoba 1, 2019 limetembelea katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam na kutoa misaada kwa wagonjwa waliolazwa wodini.
Wahariri na waandishi wa Championi walishiriki katika zoezi hilo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo pamoja na Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally.
…Akimjulia hali na kumbeba mmoja wa watoto wanaouguzwa hospitalini hapo.Timu ya Championi ilifika hospitalini hapo leo majira ya mchana na kutembelea wodi ya wazazi na watoto na kutoa misaada hiyo ikiwemo dawa, maji, juisi, pesa taslimu na vitu vingine vyenye uhitaji kwa wagonjwa hao.
Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo, Saleh Ally, alisema:
“Hii ni kampeni ambayo imeanzishwa na Gazeti la Championi, tumeanzia Hospitali ya Mwananyamala, lakini pia tutaenda sehemu tofauti kwa watu wenye mahitaji maalum.
“Haitakuwa kwenye hospitali pekee, bali hata kwenye vituo vya watoto yatima na wanamichezo, lengo ni kurudisha kwa jamii kile ambacho tunakipata.”
Awali wakati akikabidhi misaada hiyo na Timu ya Championi, Shigongo amewaasa akina mama hao waliokuwa wodini wakiuguza watoto wao na wengine wakijiuguza, kuwalea watoto wao katika misingi na maadili bora ili waje kuwa msaada kwao na taifa lao hapo baadaye.
Akizungumza ujio huo, mmoja wa akina mama hao, amelishukuru Gazeti la Championi kwa misaada hiyo na kusema kuwa jambo hilo limekuwa ni faraja kubwa kwao, hivyo wanamuomba Mungu watumiapo dawa hizo ziwasaidie, wapone na warejee nyumbani kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Mbali na kutoa misaada hiyo, Championi pia limefanya ukarabati wa jengo la Upasuaji Mkubwa (Main Theatre) katika hospitali hiyo kwa kulipaka rangi.
Championi Tuko Pamoja ni kampeni endelevu ya Championi ambayo itakuwa ikitoa misaada mbalimbali kulingana na uhitaji wa jamii.
NA MUSA MATEJA
Comments are closed.