CHANZO CHA MAUMIVU YA KIUNO NA MAGOTI

WATU wa rika zote, wanaume na wanawake husumbuliwa na tatizo la maumivu ya kiuno na magoti huku wazee ndiyo huteseka zaidi.  Tatizo huanza taratibu na wakati mwingine maumivu ya kiuno husambaa hadi magotini, lakini kwa kiasi kikubwa maumivu haya hujitegemea, yaani magoti huuma kama magoti bila ya kuhusiana na kiuno na kiuno pia huuma chenyewe.

Watu wanaosumbuliwa sana na tatizo hili mara nyingi ni wale wenye umri mkubwa hasa kina mama ambao aidha tayari wameshafikia ukomo wa hedhi au wapo katika ukomo wa hedhi kwa kuwa kiwango cha homoni ya estrojeni mwilini kinapungua na kazi ya homoni hii mojawapo ni kufanya kazi sambamba na madini ya chokaa yenye kazi ya kujenga na kuimarisha mifupa.

JINSI TATIZO LINAVYOTOKEA

Vipo vyanzo vingi vya maumivu iwe magoti au kiuno, inaweza kuwa kuumia, mfano unapoinama kunyanyua mzigo mzito au kuanguka, kufanya kazi nzito, maambukizi ya mifupa, uzito mkubwa na hata kuwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu na kansa. Kwa wanaume saratani ya tezi dume huathiri zaidi sehemu za kiuno na kuhisi maumivu ya mara kwa mara. Wanawake saratani ya shingo ya kizazi pia huchangia hali hii ya maumivu.

Maambukizi sugu au ya muda mrefu katika uzazi wa mwanamke humsababishia ahisi maumivu ya kiuno. Watu wazima au wazee ambao hapo awali walikuwa wanajishughulisha sana na baadaye wakaacha kijishughulisha hata kufanya mazoezi wapo katika hatari ya kupata tatizo hili. Kazi za kusimama muda mrefu au kutembea mwendo mrefu kama hujazoea itakupa shida. Upungufu wa ute ute wa magoti hasa kwa wazee nao husababisha maumivu na kushindwa kutembea.

Magonjwa ya mifupa, mfano baridi yabisi au gauti huchangia tatizo. Kukaa kitako muda mrefu na kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi unaweza kupata maumivu ya kiuno. Maumivu yatokanayo na maambukizi ni kama vile kifua kikuu au TB, Kaswende na endapo ulipata mivunjiko ambayo mifupa ilichomoza nje ya nyama na ukachelewa kupata tiba.

DALILI ZA TATIZO

Maumivu ya kiuno husambaa hadi magotini na unajikuta unashindwa kutembea au unatembea kwa shida. Wakati mwingine unashindwa kunyanyuka na hata kukaa kitako kiuno kinauma. Maumivu husambaa hadi juu ya mgongo na mapajani hadi katika makalio na nyuma ya mapaja. Haja kubwa unapata kwa shida na hata haja ndogo.

Magoti utashindwa kusimama vizuri, kuchuchumaa kwa taabu hata kupiga magoti huwezi. Magoti yanaweza kuvimba na wakati mwingine hujaa maji, goti linaweza kulegea na kuhama sehemu yake likiambatana na maumivu. Magoti yanaweza kuuma yote au moja. Maumivu yanaweza kuwa katika goti lote au upande.

UCHUNGUZI

Vipimo mbalimbali hufanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa. Vipimo vya damu, X-Ray na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa. Uchunguzi hufanyika katika hospitali kubwa za mikoa.

ATHARI ZA TATIZO

Maumivu ya kiuno na magoti huweza kukunyima raha muda wote, unashindwa kutembea na kushiriki shughuli mbalimbali za uzalishaji mali hata ibada, matatizo haya yanaweza kuwa ulemavu ambapo hapo awali ulikuwa mzima tu, lakini sasa ni mtu wa kutembelea kiti au kubebwa. Matatizo haya huwathiri mifumo mbalimbali ya mwili na unaweza ukajikuta unapata haja bila kujitambua au unashindwa kujizuia iwe ndogo au kubwa, unakuwa ni mtu wa kuhudumiwa, unashindwa hata kushiriki tendo la ndoa.

MATIBABU NA USHAURI

Hufanyika baada ya uchunguzi wa kina kubaini tatizo halisi kama vifupa vya kiuno vimepishana, maambukizi au kama goti limehama na mengineyo yatakayojulikana. Kwa hiyo ni vema kuwahi hospitalini kwa uchunguzi wa kina na tiba. Mgonjwa anashauriwa kuzingatia vipimo na tiba kama atakavyoshauriwa na daktari wake, zingatia mlo bora wenye virutubisho vyote. Ukizingatia tiba tatizo hili linapona vizuri.


Loading...

Toa comment