Chanzo cha ugonjwa wa Gauti na tiba yake!

GAUTI (Gout) ni aina ya ugonjwa unaoathiri viungo vya mwili unaosababishwa na kuwepo kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida cha tindikali ya Urea (uric acid) katika damu.  Ongezeko la uric acid husababisha madhara katika jointi (joint) (jointi ni sehemu ya mwili inapokutana/ inapoungana mifupa miwili).

Gauti inaweza kutokea ghafla, kitaalamu huitwa acute gout au ikawa sugu yaani chronic gout. Gauti inayotokea ghafla huwa na maumivu makali na mara nyingi huathiri jointi moja tu wakati gauti sugu inaweza kuathiri jointi zaidi ya moja na huambatana na hali ya kujirudia ya maumivu na uvimbe kwenye jointi.

Gauti husababishwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida cha uric acid katika damu. Hali hiyo hutokea iwapo mwili wa mgonjwa unatengeneza uric acid nyingi kuliko kawaida au unashindwa kutoa uric acid mwilini kama inavyotakiwa.

Ongezeko hili husababisha mrundikano wa uric acid katika majimaji yanayozunguka jointi yanayoitwa synovial fluid na hatimaye kutengeneza vijiwe vidogo vidogo vya tindikali ya urea yaani uric acid crystals ambavyo husababisha jointi kuvimba na hatimaye kuathirika.

Ingawa chanzo hakieleweki vema, ugonjwa wa gauti hutokea kuwapata baadhi ya watu walio katika familia moja. Wanaume huathiriwa zaidi kuliko wanawake ingawa wanawake waliokoma kupata hedhi huathiriwa zaidi kuliko wale wanaoendelea kupata hedhi.

Aidha unywaji pombe unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa ugonjwa huu pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile dawa za kutoa maji mwilini ambazo kwa ujumla husababisha ongezeko la kiwango cha uric acid katika damu.

Vihatarishi vingine vya gauti ni pamoja na kuwa na ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya figo, unene uliopitiliza, ugonjwa wa sickle cell anemia au aina nyingine za upungufu wa damu, pamoja na saratani ya damu (leukemia).

Hali kadhalika, gauti inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa ambazo utendaji wake kazi huingiliana na utoaji wa uric acid mwilini.

DALILI

Dalili za gauti kwa kawaida huhusisha jointi moja au jointi chache. Jointi zinazoathiriwa zaidi ni pamoja na kidole kikubwa cha mguuni, magoti au kiwiko cha mguu.

Wagonjwa huwa na maumivu yanayoanza kwa ghafla hususan nyakati za usiku. Mara nyingi mgonjwa hudai anasikia maumivu makali kama kitu kinachokata, kupwita au mifupa inayosagana. Jointi hubadilika na kuwa na joto, kuvimba na kuwa na nyekundu. Kwa kawaida mgonjwa hulalamika maumivu makali ikiwa ataguswa kwenye jointi yenye matatizo.

Shambulio linaweza kudumu kwa siku kadhaa kabla mgonjwa hajapata nafuu, lakini pia laweza kujirudia mara kwa mara. Pia mgonjwa anaweza kujihisi homa. Baadhi ya wagonjwa hupata gauti sugu ambayo huwaletea madhara sugu katika jointi hali ambayo husababisha mgonjwa kujihisi maumivu.

Wagonjwa wenye gauti kwa muda mrefu huwa pia na vinundu chini ya ngozi inayozunguka jointi zilizoathirika. Vinundu hivi kwa kitaalamu huitwa trophy na ni ishara ya muhimu kwa madaktari.

Vipimo vya gauti hujumuisha kiwango cha uric acid katika damu. Hata hivyo, si kila aliye na kiwango kikubwa cha uric acid katika damu huwa na gauti. Mtu anaweza kufanyiwa uchunguzi wa maji maji yanayozunguka jointi kuchunguza vijiwe katika jointi, X ray ya jointi iliyoathirika au uchunguzi wa utando unaozunguka jointi.

MATIBABU

Matibabu ya gauti hujumuisha matumizi ya dawa, lishe pamoja na mabadiliko katika mfumo wa maisha wa mgonjwa. Dawa hutumika mara tu mgonjwa anapopata shambulio la ghafla. Dawa hizo ni pamoja na za kutuliza maumivu kama vile codeine, paracetamol, za kutuliza mcharuko mwili.

USHAURI

Wagonjwa wanaofuata masharti na ushauri wa daktari huweza kuishi maisha ya kawaida. Hata hivyo, ni vema kufahamu kuwa mara nyingi gauti ya ghafla hatimaye huwa gauti sugu.


Loading...

Toa comment