
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, .John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, katika Ikulu Ndogo ya Chato Mkoa wa Geita.
Maalim amefika mapema leo Januari, 14, 2021, katika uwanja wa ndege wa Mwanza na kupokelewa na viongozi waandamizi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Mkoa wa Mwanza, Sevelin Lalika.

Pia alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa Daraja la Magufuli lililopo Kigongo Feri mpakani mwa Misungwi na Sengerema.
Mradi wa daraja hilo ukikamilika utaleta mafanikio makubwa ya kuunganisha baadhi mikoa ya Tanzania na kuunganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Congo.

Baada ya ziara hio Maalim Seif alikwenda Chato kukutana na marais hao ambapo walijadili mambo mengi na baadaye kuzungumza na umma wa Watanzania na dunia kwa jumla kupitia waandishi wa habari.
Katika mkutano huo Maalim alisema: ”Tumebadilishana mawazo juu ya mustakabali wetu wa Zanzibar na namna bora zaidi ambavyo tunaweza kuwatumikia Watanzania.

“Kwa namna tulivyozungumza na kukubaliana inaonyesha wazi Rais Magufuli ana nia njema ya kutuunga mkono na kuyaboresha maisha ya Wazanzibar wa visiwa vya Pemba na Unguja.”

