The House of Favourite Newspapers

Chatu, Chui, Mamba Wazua Kizaazaa Mtaani Dar

0
Diwani Muharijani Kassim Obama akiongea na Global TV eneo la tukio lililovamiwa na wanyama.

TAHARUKI kubwa imeibuka kwa wakazi wa eneo la Kitunda Mtaa wa Bunju B, Kata ya Mabwepande, Kinondoni, jijini Dar es Salaam baada ya wanyama wakali kudaiwa kuonekana katika makazi yao.

Wananchi wakiwa wamejikusanya kumsubiri diwani wao Obama.

Wanyama hao waliodaiwa kuonekana katika eneo hilo ni chatu, chui na mamba ambao wamewalazimisha wakazi hao wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Mabwepande, Muharijani Kassim kuwasaka wanyama hao na kufanya usafi katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Bunju B, Athumani Njama akizungumza eneo la tukio.

Wakizungumza na gazeto ;a Amani kupitia diwani huyo maarufu kama Obama, wameiomba serikali kuwasaidia baada ya kuishi kwa hofu hasa baada ya kumshuhudia chatu mmoja  akimmeza mbwa wao. Katika mkutano ulioitishwa na Obama,  ulianza kwa wananchi hao kufanya usafi katika eneo itakapojengwa Shule ya Msingi Bunju B ambapo walifyeka eneo hilo ili kuanza ujenzi. Akizungumza na wananchi hao,  Kassim alisema anaamini serikali ni sikivu na itawasaidia kukabiliana na tishio la chatu hao wanaodaiwa kuzagaa mtaani.

Obama akiwatuliza wananchi kuhusiana na tishio la wanyama hao pamoja na kuwaahidi kumaliza mgogoro wa nyumba zao.

Obama alisema chanzo cha kuzaliana kwa chatu na wanyama wakali katika eneo hilo ni kuwepo kwa pori ambalo lina mgogoro kwa miaka zaidi ya saba. Alisema pori hili liko karibu na eneo ambalo shule ya msingi itajengwa, hivyo kuiomba serikali kuingilia kati ili kesi ya mgogoro wa eneo hilo iliyopo Mahakama Kuu ya Ardhi imalizike.

 

“Hatuna mamlaka ya kuingilia kati kesi ila tutaiandikia maombi mahakama ituruhusu kufyeka eneo hili ili kuepusha chatu kuzaliana,”alieleza Obama.

Katibu wa CCM Kata ya Bunju B, Mariam Shomari akizungumza eneo la tukio.

Alisema tayari Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imetoa sh. milioni 156 kujenga madarasa tisa katika eneo hilo.

 

“Hatuna shule hapa Kitunda, shule ipo upande wa pili wa Barabara ya Bagamoyo, Mtaa wa Kiyonzile, hivyo ujenzi wa shule hii mpya ni muhimu ili kuepusha watoto kugongwa na magari au tishio hili la chatu na wanyama wakali. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bunju B, Athuman Njama, alithibitisha wananchi wake kuishi katika tishio la chatu hao aliodai wanaranda mara kwa mara mtaani.

Estrida Sauli mkazi wa eneo hilo akielezea jinsi watoto wake wanavyoshindwa kwenda shuleni kufuatia tishio la wanyama hao.

“Wananchi wanaishi kwa hofu hapa.Wengi wanajifungia mapema ndani,” alisema Njama  akiongeza: “Tunaomba serikali ije itusaidie kuwinda wanyama hawa.”

 

Mzee Asheli Ishiriyo, mkazi wa eneo hilo alisema hivi karibuni chatu mkubwa alikutwa akimmeza mbwa katika banda la jirani yake.

 

“Alikuwa ni mkubwa kama nguzo ya umeme.  Alipotuona alimtema mbwa na kutuvimbia ili kukabiliana na sisi. Tukakimbia,”alieleza mzee huyo.

 

Naye, Ally Said, alisema mwezi mmoja uliopita walifanikiwa kumuua chatu mmoja na kumfukia.

Hili ndilo eneo linalodaiwa kuwa na wanyama hao.

 

HABARI/PICHA ZOTE NA RICHARD BUKOS /GPL

Leave A Reply