The House of Favourite Newspapers

Chavita kuadhimisha wiki ya viziwi duniani

0

Ofisa wa jinsia na Maendeleo kutoka makao makuu ya Chama  cha Viziwi Tanzania (Chavita), Lupia Mwaisaka,(kushoto) akizungumza kwa kutumia ishara ya mikono.  Kulia kwake ni baadhi ya viongozi wenzake wa chama hicho wakiwa kwenye mkutano huo.

Jane Malumbo  (kulia) ambaye ni mkalimani wa kutafsiri lugha ya alama aliyokuwa akizungumza, Lupia Mwaisaka,  akirekodiwa na wanahabari mbele ya viongozi hao.

…Akionesha msisitizo wa jambo (katikati).

CHAMA cha Viziwi Tanzania (Chavita) kupitia tawi la Mkoa wa Pwani na asasi mbalimbali za viziwi na zile zinazotoa huduma kwa ajili yao zimepanga kuadhimisha Wiki ya Viziwi Duniani Septemba 27 mwaka huu.

Chama cha viziwi hujumuisha taasisi za shule za viziwi, wazazi viziwi, wasanii viziwi, CCBRT, shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), vyama vyenye watu wenye ulemavu (DPOs) na wadau wengine.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es salaam, ofisa jinsia na maendeleo kutoka makao makuu ya chama hicho (Chavita),Lupia Mwaisaka, akisaidiwa kutafsiri na mkalimani wake, Jane Malumbo, amesema  maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 27 mwaka huu kwenye viwanja vya Bwawani Kibaha Maili Moja yakitanguliwa na matembezi ya mshikamano kuanzia kwenye viwanja vya TAMCO, kuelekea Kibaha mjini.

Amesema kuwa lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kujenga mwamko wa jamii kuhusu haki za viziwi hususani utambuzi rasmi  wa lugha ya alama kama njia ya mawasiliano kwa viziwi na fursa ya watoto viziwi katika maendeleo ya kielimu, kukuza vipaji na kuweza kutimiza ndoto zao wakiwa kama sehemu ya nchi.

Alizidi kufafanua kuwa siku hiyo kwao itaweza kuwakutanisha  viziwi na wanataaluma mbalimbali kujadili changamoto zinazowakabili kupitia vyombo  vya habari, na kutoa fursa kwa jamii kuona namna wanavyoweza kuondokana na changamoto hiyo ya upatikanaji wa taarifa kamili kutoka kwenye vyombo vya habari kwa kuwawekea mkalimani.

Aliongeza mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid  akaongeza kuwa  wiki ya kimataifa ya viziwi huongeza mshikamano miongoni mwao na washirika wao na ikitumika kama njia ya kuonesha na kuchochea jitihada zaidi katika kuendeleza haki za binadamu kwa viziwi.

Aidha maadhimisho hayo yanaenda na kaulimbiu isemayo  ”Kwa haki za lugha ya alama ya Tanzania, watoto wetu wanaweza”.  Kauli hiyo inalenga kuhamasisha na kutambua mchango wa viziwi katika maeneo mbalimbali duniani, haki za binadamu katika kukabiliana na changamoto za maisha yao ya baadae.

Hata hivyo alisema  siku ya maadhimisho ya wiki ya viziwi ni moja ya kumbukumbuu ya kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa Shirikisho la Viziwi Duniani (WFD) uliofanyika Septemba 1951 mjini Rome Italia.

(NA DENIS MTIMA/GPL)

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS UPATE HABARI KEMKEM ZA UCHAGUZI MKUU

globalbreakingnews.JPG

Leave A Reply