The House of Favourite Newspapers

Chelsea Yasajili Straika Wa Juventus Kwa Mkopo

 

KLABU  ya Chelsea ya Uingereza imemsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Juventus. ‘Gonzalo Higuain’. mpaka mwisho wa msimu.

 

Miamba hiyo ya London pia ina nafasi ya kumsajili moja kwa moja kwa kima cha pauni milioni 31.3. Kuna uwezekano pia wa kuongeza mkataba huo wa mkopo mpaka Juni 2020 lakini itawapasa kutoa kitita cha pauni milioni 15.

 

Higuain, 31, ambaye ni raia wa Argentina amecheza nusu ya kwanza ya msimu huu kwa mkopo katika klabu ya AC Milan, na kufunga magoli manane kwenye michezo 22.

 

“Pale fursa ya kujiunga na Chelsea ilipojitokeza ilinibidi niichangamkie,” amesema Higuain na kuongeza:

 

“Ni timu ambayo nimekuwa nikiipenda na ina historia pana, uwanja mzuri na inashiriki Ligi ya Premia ambayo nimekuwa nikiitamani kila siku kuicheza.”

 

Kutokana na usajili huo kufanyika baada ya saa sita usiku ya Jumatano, Higuain hataweza kuichezea klabu yake mpya kwenye mechi ya nusu fainali ya pili ya Kombe la Corabao usiku wa leo dhidi ya Tottenham.

 

Straika huyo alicheza chini ya kocha wa sasa wa Chelsea, Maurizio Sarri, katika klabu ya Napoli msimu wa 2015-16, na kufikia rekodi ya kutikisa nyavu kwa wingi katika ligi ya Serie A baada ya kufunga mabao 36.

 

“Ni mshambuliaji mwenye nguvu, alidhihirisha hilo katika msimu wangu wa kwanza na Napoli,” amesema Sarri na kuongeza: “Alifanya vizuri sana. Kwa hakika, yeye ni mmoja wa washambuliaji magwiji zaidi ambao nimewahi kufanya nao kazi.

 

“Ninaamini ataanza tena kushinda na timu yetu. Najua amekumbwa na ukame kwa sasa.”

 

Higuain ameongeza kuwa: “Sasa nina imani nitaweza kuilipa Chelsea uwanjani kwa imani walioinesha kwangu. Nina hamu kubwa ya kuanza kucheza na naamini nitazoea mazingira kwa haraka iwezekanavyo.”

 

Mkurugenzi wa Chelsea Marina Granovskaia amesema Higuain ndio alikuwa kipaumbele chao cha kwanza katika dirisha la usajili la mwezi Januari na amewasilia kiwa na “rekodi iliyodhihiri (ya kucheza) katika kiwango cha juu”.

 

“Ameshafanya kazi hapo awali na Maurizio kwa ufanisi mkubwa na anajua kocha wake anapendelea mchezo wa aina gani,” ameongeza Granovskaia.

 

“Huu haukuwa usajili mwepesi kwetu sababu kulikuwa na wahusika wengi, lakini tunafuraha kuona kuwa tumeweza.”

 

Higuain alihushwa na tetesi za kuhamia klabu ya Arsenal kabla ya Juventus kumsajili kwa dau liloweka rekodi nchini Italia la pauni milioni 75.3 akitokea Napoli Julai 2016.

 

Baada ya kucheka na nyavu mara 40 kwa misimu miwili na Juventus, alihamia AC Milan kwa mkopo mwezi Agosti. Kulikuwa na fursa kwa Milan kumbakisha mwisho wa msimu huu kwa dau la pauni milioni 36.

 

Alianza kwa kiwango cha juu maisha yake na Milan kwa kufunga magoli sita katika mechi tano za mwanzo, hata hivyo amefunga goli moja tu kwenye michezo 12 iliyopita.

 

Chelsea kwa sasa ipo katika nafasi ya nne katika msimao wa Ligi ya Premia, wakiwa na alama tatu juu ya mahasimu wao Arsenal ambao waliwafunga 2-0 siku ya Jumamosi.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.