CHEZEA KOKI YA MAJI, USICHEZEE PESA

BINADAMU bwana! Hata ukiogelea watasema unawatimulia vumbi, haloooo ehhhhh! Unashanga, hebu kashangae basi memori kadi ndogo lakini inailiza sabuufa! Heheiyaaaa! Haya wewe uliyekuja kwa gari la mkaa, juu mpaka chini hujulikani hata rangi yako ni halisi ama ni mkorogo! Waareeeee reeee! Shoga wanakwambia ukimuona ngedere mjini basi ujue ana mwenyewe, Anti Naa ndiyo nimekuja tena maana huchelewi kuchamba wakati hata kutumia maji huwezi, upo?

Kama umeangalia kalenda, simaanishi zile kalenda zetu kama nakuona kusikia kalenda moja kwa moja akili yako inakupeleka kwenye usichana, looo! Shoga naongelea kalenda hii unayoijua, kama ulikuwa hujui jua sasa, huu ndiyo mwezi wa mwisho wa mwaka! Mwanamke unatakiwa ujitambue kuwa sasa tunaelekea kufunga mwaka na hakuna mwezi mgumu kama ule unaofuatia, matatizo yanakuwa mengi, basi ifike wakati tumsaidie hata baba kwenye majukumu. Kama unaona anafuja pesa kipindi hiki ndiyo mahali pa kumuonesha umuhimu wako, au siyo nyonyo?

Wanakwambia mbwa mwenye mnofu hawezi kupiga kelele, hilo sikatai, wakati mwingine sisi wanawake tukishaona baba amepata kiasi fulani, ukiangalia sikukuu hizi, jicho na mate yote yatakutoka kwenye kuvaa, kula na kufanya matanuzi yasiyokuwa na maana! Tena wengine wanaenda mbali kwa kuwaiga majirani wakati pesa zao za msimu, heee heeeiyaaaa!

Shoga afadhali kuchakaza nguo kuliko pesa, siyo lazima kuiga maisha ya mwenzako! Kama huna huna tu, kwaaaani ukisema ujibane hiyo pesa ikashonea watoto wako sare za shule na manunuzi mengine ya shule pamoja na ada zao utakuwa umekosa nini?

Kawaida yangu nikisemaga huwa namaanisha ati! Nimekuwa mzoefu wa kupokea malalamiko mengi baada ya mwezi huu kuisha si mwanaume wala mwanamke analalamika oohh, mwezi umekuwa mgumu, nikifikiria watoto nachanganyikiwa, bado wakwe wananisumbua, kodi ya nyumba ndiyo usiseme! Anasahau kabisa kuwa mwezi Desemba alichakaza pesa na sasa zinamchakaza yeye! Mshiiiiiuuuuuuu!

Katika maisha shoga yangu ni bora ukacheza na koki ya bomba itakulowesha na mwisho wa siku itakaa sawa lakini ukicheza na pesa kinachotokeaga huwa ni majuto, upo nyonyo? Nakukumbusha mwezi huu ndiyo kwanza mbichi na sikukuu zitaanza kufululiza mwishoni mwa mwaka, kabla ya kufanya matanuzi ya familia kwanza jitathimini shoga mwezi unaofuatia utaweza kufanya yote yatakayowazunguka?

Nisiwe muongeaji sana, nimeyatapika yale yote yaliyonikaa, yafanyie kazi shoga uvuke salama mwezi ujao! Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri! Ni mimi Anti Nasra ukipenda niite Shangingi Mstaafu!

Loading...

Toa comment