The House of Favourite Newspapers

Chid Benz amka, turudishe kwenye ubora wako!

0

1 Rashid Abdallah Makwiro ‘Chid Benz’.

KWAKO mkali wao, mbabe wao, Rashid Abdallah Makwiro ‘Chid Benz’ habari yako kaka? Vipi upo? Za masiku? Unajionaje na hali? Ilala mnatunyima nini?
Mimi ni mzima, namshukuru Mungu. Naendelea kupambana na shughuli zangu za kila siku. Naendelea kuandika maana ndiyo kazi inayonipatia ugali. Kukuandikia hii barua pia ni sehemu ya kazi yangu.

Nimekukumbuka ndugu yangu kutokana na kukumisi katika anga la muziki. Nimemisi ule uwezo wako mkubwa wa kunata na biti huku ukiwa na ‘voko’ lililoshiba kwelikweli.
Zamani walikupa majina mengi kutokana na kipaji chako cha kuchana mashairi ya Hip Hop. Hadi leo nakumbuka wimbo wako wa taifa, Dar es Salaam Stand Up.

Huu ulikuwa gumzo. Ulipendwa na kila mtu. Ulikaza kwelikweli. Nakumbuka enzi hizo ndiyo ulikuwa wa gharama sana, watu kibao walikuomba kolabo, ulikuwa king wa kolabo.
Madhumuni ya kukuandikia barua hii mbali na kukukumbuka, nataka kujua kwa nini umekubali muziki ukuache nyuma wakati uwezo unao.

Nikiitazama sauti yako, uwezo wako wa kughani mashairi ya papo kwa hapo (freestyle), wewe ni zaidi ya msanii. Ni zaidi ya Muziki wa Bongo Fleva, unapaswa kuwa juu kama walivyo akina MwanaFA na AY ambao wameanza gemu kitambo lakini hadi leo tunaendelea kuwasikia katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni.
Natambua kwamba katika harakati za maisha ulitajwa kushiriki vilevi hatari vilivyokufanya utoke kwenye reli lakini mwenye nafasi ya kurudi katika ubora wako ni wewe mwenyewe.

Amua sasa. Kama bado unaendelea kutumia yale mambo, achana nayo. Yanakuharibia maisha yako. Waone wataalamu watakuelekeza namna ya kuacha. Heshima uliyoitengeneza kwa muda mrefu kwa nini ipotee kama kuzima taa?
Kwani kuimba ni mzigo? Kipaji kimezeeka? Mimi naamini unaweza kuingia studio, unaweza bado kuimba nyimbo nzuri na mashabiki wakakumbuka zile enzi za Dar es Salaam Stand Up.

Naamini bado unaweza kupata mameneja wazuri ambao wataweza kuusimamia muziki wako kama wewe utaonesha ‘u-serious’. Wewe ni bidhaa. Hakuna asiyejua kwamba akifanya kazi na wewe atapata faida.

Japo waswahili wanasema mara nyingi ukishaanguka kuinuka ni vigumu lakini mimi naamini wewe unaweza. Ukiamua unaweza kuturudisha kwenye ubora wako, ukaimba muziki mzuri na mashabiki wakaendelea kukusapoti kama zamani.
Pamoja na wewe kuamua lakini nikushauri, kwa imani yako muombe Mungu akusaidie ili uweze kurudi katika mstari.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na utaufanyia kazi ushauri wangu. Nikutakie utekelezaji mwema.

Wako katika ujenzi wa sanaa yetu;
Erick Evarist

Leave A Reply