CHID BENZ: ISHU YA MADAWA NI KIKI?

CHID BENZ: ISHU YA MADAWA NI KIK

Rashid Makwiro ‘Chid Benz’.

MWANZONI mwa mwezi Julai, mwanamuziki mwenye jina kubwa kwenye tasnia ya Muziki wa Hip Hop, Bongo, Rashid Makwiro ‘Chid Benz’ alifanya ‘media tour’ kuutambulisha wimbo wake mpya uitwao Muda akiwa na Abubakar Katwila ‘Q Chillah’, aliyemshirikisha kwenye wimbo huo. Chid Benz alifanya tour hiyo ukiwa ni muda mchache tu baada ya kutoka kwenye kituo kimoja cha kusaidia waathirika wa dawa za kulevya (soba) kilichopo mkoani Iringa.

Katika tour hiyo miongoni mwa maswali aliyokutana nayo wakati akitambulisha wimbo wake wa muda ni juu ya hatima yake na matumizi ya dawa za kulevya ambayo alikuwa ametopea. Chid Benz akasema-nanukuu kutoka kwenye mahojiano yake na redio moja kwamba- hataki kuzungumzia ishu ya yeye na dawa za kulevya kwa maana ameshatoka kwenye ulimwengu huo.

Anachotaka kusikia ni juu ya wimbo wake wa Muda, na kuwa ndiyo amerudi hivyo kwenye gemu la muziki Bongo kufuta vumbi kwenye kiti chake. Jambo la kushangaza zaidi ukiachana na tetesi za Chid kuhemea unga maeneo ya Jangwani, Dar kwa mapusha, mkali huyo wiki mbili zilizopita alidakwa kwa ishu ya unga na kuswekwa kwenye Kituo cha Polisi Msimbazi.

Chid ametoka na muda mfupi tu baada ya kuachiwa ameachia video ya wimbo wake wa Muda! Sasa swali kwa Chid Benz, ishu ya dawa za kulevya kwake ni kiki? Kwamba akitaka kufanya lolote lile ni lazima tumsikie na misukosuko ya dawa za kulevya halafu ndiyo tumpokee? Anahitaji maombi ya Watanzania ama huruma yao mpaka lini ikiwa yeye mwenyewe hayupo tayari kuachana na dawa za kulevya?

Msikie huyu hapa nikifanya naye mahojiano;

Showbiz Extra: Vipi Chid? Benz: Poa tu, mzigo ndiyo huo nimeuachia. Mashabiki wangu muda mrefu walikuwa wanazungumza kuhusu video hatimaye nimeitoa kwa hiyo nahitaji sapoti yao.

Showbiz Extra: Sawa. Bila shaka sapoti utapata. Kwa sasa nani anasimamia kazi zako? Chid Benz: Ni mimi mwenyewe na baadhi ya watu wangu wa karibu.

Showbiz Extra: Sawa, na hili la wewe kukamatwa na dawa za kulevya liko vipi? Ni kiki ya kutoka na video ya wimbo au kuna ukweli upi ambao umejificha ikizingatiwa wewe umewahi kukiri mara kadhaa kuachana na dawa za kulevya?

Chid Benz: Kuhusu hilo nina ushauri kutoka kwa mama watoto wangu kwamba nisilizungumzie zaidi. Lakini kwa ufupi ni kwamba mtu kukamatwa na dawa za kulevya ni sawa na mtu aliyekamatwa na bangi, mirungi ama chochote kile ambacho
kinaonekana kuvunja sheria za nchi!

Kwa hiyo nisiingie huko sana lakini jambo la msingi ni kwamba vijana wa Kitanzania wasijaribu na wanaotumia dawa za kulevya waachane nazo, siyo nzuri zaidi wajenge taifa kwa manufaa ya kizazi chetu.

Showbiz Extra: Umekuwa ukiwaeleza mara kwa mara mashabiki wako kwamba unaachana na unga lakini misukosuko ya unga haikuachi salama labda hili umejipanga vipi kukabiliana nalo?

Chid Benz: Nishakabiliana nazo hizo changamoto na sidhani kama zitajirudia tena. Ishu ya msingi maswali ya Chid Benz na unga tuachane nayo, tumpokee Chid Benz na video ya wimbo wake wa Muda.

Showbiz Extra: Mbali na kutoa video hii umejipanga vipi kuhakikisha unakabiliana na changamoto za vijana wanaofanya vizuri kwa sasa kwenye gemu?

Chid Benz: Nafikiri Chid Benz hawezi kuzuia wanamuziki kufanya vizuri, kikubwa ni kwamba nafasi yake ipo palepale. Kwa hiyo sina shaka na hilo na mashabiki wangu wanipokee tu.

Showbiz Extra: Ukiachana na ujio huu ujio mpya, umeshajipanga na wimbo mwingine na pengine unategemea kuufanyia wapi au kuufanya na nani?

Chid Benz: Mipango ipo mingi sana na siwezi kuizungumza kwa sasa. Kikubwa tuusapoti huu wimbo na ukifika muda wa ujio mpya kila kitu kitakuwa wazi.

Showbiz Extra: Nakushukuru kwa ushirikiano pengine malizia na neno kwa mashabiki wa kazi zako.

Chid Benz: Kwa mashabiki wangu nawapenda. Na waendelee kusapoti kazi zangu na waamini kwamba nimejifunza kutokana na mambo yaliyopita na kwa sasa nipo kwa ajili ya kufanya kazi basi!

 

NA: BONIPHACE NGUMIJE| AMANI


Loading...

Toa comment