The House of Favourite Newspapers

CHIMBO LA MASTAA WABWIA UNGA LANASWA

0
MASTAA WABWIA UNGA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

HILI ni janga! Miezi kadhaa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuchimba mkwara mzito kwa watumiaji na wauzaji wa madawa ya kulevya, juzikati limebainika chimbo ambalo baadhi ya mastaa Bongo hufika kwa ajili ya kupata kilevi hicho haramu, Ijumaa limeingia mzigoni.

 

NI KARIAKOO- JANGWANI

Chanzo chetu kinachoishi maeneo ya Jangwani, Kariakoo jijini Dar wiki mbili nyuma kilipiga simu na kueleza kuwa, katika maeneo hayo lipo chimbo ambalo watu wengi wakiwemo mastaa hufika na kuuziwa unga kwa usiri mkubwa hasa nyakati za usiku.

 

“Ni mitaa flani ya hapahapa Jangwani karibu na kanisa moja la Kiroho, wanakuja wengi tu, wanawake na wanaume. Njooni mjionee wenyewe ili mumfikishie hizi taarifa mkuu wetu wa mkoa. Jitihada zake bado kuna wanaozirudisha nyuma. Ila chondechonde msinitaje maana anayewauzia ni mmafia,” alitiririka mtoa habari huyo.

 

CHID BENZ AONEKANA USIKU

Kuonesha kuwa chanzo hicho kiko makini, siku mbili mbele kilipiga tena simu saa 1.30 usiku na kueleza kuwa, msanii maarufu aliyewahi kukiri kwamba ameacha kutumia unga, Rashidi Makwiro ‘Chid Benz’ yupo mitaa hiyo akiwa na watu wengine ambao hawakufahamika majina yao.

MASTAA WABWIA UNGA
Rashidi Makwiro ‘Chid Benz’.

“Jamani kama mnaweza kuwahi njooni fasta leo mumshuhudie Chid Benz, yupo hapa na watu wengine, wanaoonekana kama mastaa flani. Kuna na binti mmoja ni msanii kavaa baibui, njooni fasta,” kilinyetisha chanzo hicho kwa msisitizo kikiamini kuwa, habari hiyo ikipatikana kitapata mkwanja.

 

MAPAPARAZI WATINGA ENEO LA TUKIO

Ili kuweza kuipata habari hiyo, mapaparazi wetu walichukua usafiri wa bodaboda kutoka Mwenge lakini walipofika Jangwani, ‘mateja’ hao walikuwa wameshaondoka.

 

KAMBI YAWEKWA

Kwa kuamini kuwa, kwa mtumiaji wa unga haiwezi kupita siku bila ‘kubembea’, waandishi wetu waliamua kuweka kambi katika eneo hilo kwa siku kadhaa lakini hawakufanikiwa kuwanasa mastaa zaidi ya watu wa kawaida waliokuwa wakionekana wakifika na kuondoka.

 

POLISI WAMDAKA CHID BENZ

Kana kwamba polisi nao walikuwa wameshalishtukia chimbo hilo, Jumamosi iliyopita ilidaiwa kuwa Chid Benz akiwa na watu wengine 5 walidakwa na polisi wakiwa na madawa ya kulevya. Chanzo kilekile ambacho kinaishi maeneo hayo ndicho kilichoturushia habari hiyo na kueleza kuwa, baada ya staa huyo akiwa na wenzake kukamatwa walipelekwa Kituo cha Polisi Msimbazi ambako walilala kwa zaidi ya siku tatu. Ikazidi kuelezwa kuwa, Chid alikamatwa na kulazwa selo kwa siku zote hizo ili kufanikisha kukamatwa kwa mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Abedi ambaye ndiye anayedaiwa kuwauzia.

 

“Huyo Abedi ni maarufu sana eneo hili na alikuwemo kwenye ile listi ya Makonda ya vigogo wanaouza unga. Si unajua unga sasa hivi ni shida sana kuupata, sasa yeye kaamua kujilipua hivyo wale ambao wameshindwa kuacha ndio wanakuja pale kutoka maeneo mbalimbali, kimsingi ni chimbo ambalo kama hulijui vizuri huwezi kuamini kama mastaa wanaweza kuwa wanafika,” alisema mtoa habari wetu.

 

MAENEO YAKOJE

Waandishi wetu wakiwa eneo hilo walifanikiwa kupiga picha mbalimbali zikiwaonesha baadhi ya watu wanaodaiwa ni watumiaji wa unga na bangi wakiwa kwenye chimbo hilo huku ikielezwa kuwa, ukienda kichwakichwa kwa nia ya kuwalipua ni rahisi kufanyiwa kitu mbaya. Hata hivyo, uchunguzi
wetu umebaini kuwa, baada ya akina Chid Benz kukamatwa, aliyekuwa akiwauzia ameingia mitini na biashara ya unga eneo hilo ni kama ‘imeingia shubiri’ kwa kuwa polisi kila dakika wanapita.

MASTAA WABWIA UNGA
Eneo linalodaiwa kuwa Chimbo la madawa ya kulevya.

TUMEFIKAJE HAPA?

Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda alitangaza azma yake ya kupambana na biashara ya madawa ya kulevya ambapo aliwataja wanaodaiwa kuuza na kutumia. Kwenye listi ya mastaa waliotajwa kutumia madawa ya kulevya walikuwemo Rommy Jones, Khalid Mohammed ‘TID’, Gedou Mandingo ‘Babuu wa Kitaa’, Ahmed Hashim ‘Petit Man’ Anna Kimario ‘Tunda’, Rachel Josephat na wengine ambao walipofikishwa mahakamani walikiri na kuahidi kuachana na ulevi huo.

 

Hata hivyo, gazeti hili linawafuatilia mastaa hao ili kubaini kama kweli wameacha na siku chache zijazo ripoti ya wote waliokuwa wakitumia unga itakuwa kwenye kurasa za gazeti hili. Mbali na hao, Wema Sepetu na Agnes Gerald ‘Masogange’ kesi zao wakituhumiwa kutumia madawa ya kulevya bado zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.

 

KUTOKA IJUMAA

Gazeti hili linaunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya na kuwataka mastaa na watu wengine wa kawaida wanaoendelea kutumia na kuuza kuacha kwani madhara yake ni makubwa kikiwemo kifo.

 

STORI: BONIPHACE NGUMIJE NA ALLY KAALAMBULA| IJUMAA

Leave A Reply