China Yatangaza kuongeza ushuru wa bidhaa zinazotoka Marekani
Serikali ya China leo, Jumanne Februari 4, 2025, imetangaza kuongeza ushuru wa bidhaa zinazotoka Marekani kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya sheria mpya ya Marekani ya kuongeza ushuru kwa bidhaa za China kwa asilimia 10 kuanza kutumika.
Awali, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kuongeza ushuru kwa bidhaa za China zinazoingia Marekani kwa asilimia 10, kama shinikizo la kuitaka China kuacha kuingiza dawa bandia nchini Marekani.
Waziri wa Fedha wa China amenukuliwa akisema kuwa bidhaa zitakazoongezewa kodi zinajumuisha makaa ya mawe, gesi asilia, mafuta ghafi, vifaa vya mashambani pamoja na magari makubwa.
Bidhaa nyingine ni pamoja na magari ya umeme yanayozalishwa na Kampuni ya Tesla, inayomilikiwa na swahiba wa karibu wa Trump, Elon Musk.
China pia imeongeza kuwa inazifanyia uchunguzi kampuni za Kimarekani kama Google, PVH Corp inayomiliki chapa ya Calvin Klein, na kampuni ya dawa ya Illumina, na endapo zitapatikana na hatia, zitafungiwa nchini China.