The House of Favourite Newspapers

Choki Apania Kuweka Rekodi Mpya Tamasha la Miaka 30 ya Uimbaji Wake

 choki 

MWIMBAJI maarufu na mkongwe kwenye muziki wa dansi, Ali Choki (pichani juu) ameeleza kuwa atafanya makamuzi ya hatari kwenye tamasha la kutimiza miaka 30 ya uimbaji tangu kuanza kwake kazi hiyo.

Akichonga na Global TV Online, Choki amesema kuwa tamasha hilo limepangwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mango Garden jijini Dar es Salaam huku akiahidi kufanya makubwa ikiwa ni pamoja na kuweka rekodi mpya kwa kufanya shoo mpya na ya kisasa zaidi.

“Mimi nimeanza kazi ya muziki mwaka 1986 nikiwa shule kule Bagamoyo, Pwani. Bendi yangu ya kwanza kufanya nayo kazi ilikuwa ni Bagamoyo Sound na nimefanya muziki na watu wengi maarufu na wa kawaida, wazee kwa vijana, nimepitia mengi sana kwenye muziki huu mpaka kuufikisha hapo ulipo. Hivyo nimeona ni vyema kufanya tamasha la kuadhimisha miaka 30 ya kazi yangu. Kwenye tamasha hilo nimewaalika wasanii wengi wakongwe, wa Bongo Fleva na wa Singeli wote watagonga shoo. Nimepania kufanya makubwa sana kwenye shoo hiyo kwani tuna vifaa vya kisasa pia tumejiandaa kikamilifu na tunaendelea kujiandaa”, alisema Choki.

choki-4

Choki akipozi na Mhariri wa Gazeti la Championi Ijumaa, John Joseph alipotembelea studio za  Global TV Online.

Mbali na kufanya shoo, Choki ameeleza kuwa siku hiyo atatambulisha na kuachia wimbo wake mpya ambao anadai ameufanya kwa umakini na ubunifu mkubwa tofauti na nyimbo zake za mwanzo.

Staa huyo pia amewondoa wasiwasi mashabiki zake kutokana na taarifa zinazosambazwa kuwa kuna bendi kubwa inataka kumchukua ili aihame Twanga Pepeta. “Naomba niwatoe hofu mashabiki wangu na wadau wa muziki wa dansi, bado nina mkataba na Twanga Pepeta hadi mwaka 2018, sasa anayeongea kuwa mimi nataka kuondoka Twanga mimi sielewi anaambiwa na nani? Anafahamu habari zangu wakati mimi sizijui?”, alihoji Choki na kuonesha kusikitishwa na maneno hayo huku akiwataka wadau wa muziki wa dansi wayapuuze kwamba si ya kweli na kwamba yeye yupo Twanga na ataendelea kuwepo Twanga.

Na Edwin Lindege/GPL

Comments are closed.