The House of Favourite Newspapers

Chongo!-12

0

Ilipoishia wiki iliyopita
“Safi sana, hebu tuambie ulikuwa unakaa wapi? Noel alimwuliza Bata, ambaye hadi wakati huo walikuwa hawajui jina lake.
“Kwani hapa tulipo ni wapi?” Bata aliwauliza akionekana kuwa na hamu sana ya kujua!
“Hapa ni Tegeta Magereji,”
“Tegeta?”
Sasa endelea…

“Ndiyo, hapa ni Tegeta Magereji, upande huu ni Madale, kama unaenda hivi ni Boko, Bunju hadi Bagamoyo, huku ni Mbezi hadi Kariakoo, wewe ulikuwa unakaa wapi?” Noel alimwuliza.
Kijana huyo alinyamaza ghafla na kuanza kufikiria kwa umakini, kichwani mwake alirejewa na fahamu kuwa Tegeta haikuwa mbali na nyumbani kwao, lakini ni wapi hasa hilo hakuweza kulibaini mapema. Aliwatazama wenyeji wake huku akionekana kabisa kukumbuka kitu, jambo ambalo hata akina Noel na mzee Masta walilibaini.
Kuona hivyo, wakatazamana na kupeana ishara ya kubadili mazungumzo ili kumuweka sawa, wakarukia topiki nyingine ambayo baadaye Bata naye alijiunga nao. Walikaa pale wakizungumza hadi ilipofika saa kumi na mbili jioni mtoto yule alipoomba kwenda kulala. Wakamruhusu.
Maisha yaliendelea vile kwa miezi kadhaa, Bata akipelekwa hospitalini kuchunguzwa maendeleo ya afya yake. Kila mara alielezwa kuimarika misuli ya kichwa na hata kasi ya kurejea kwa kumbukumbu yake nayo ilikwenda vizuri.
**
Jerry alikaa Durban kwa miezi kama mitatu, kila siku akiwasiliana na mpenzi wake kujua nini kilichokuwa kikiendelea, lakini mara zote ikaonekana kuwa hakukuwa na dalili za kuonekana kwa Bata wala kupata habari zake. Hali hiyo ilizidisha hofu kwao, kwani walihitaji kupata uhakika wa kama yuko hai au la.
Katika mashauriano yao, Jerry na Ame wakakubaliana kuhamia Afrika Kusini. Kwa kuanzia, Ame akauza maduka yote makubwa ya vifaa vya ujenzi, kitu alichokifanya siri, pasipo ndugu zake kufahamu. Hata hivyo, wasingeweza kufanya lolote endapo wangejua, ingawa wangemsengenya.
Alipata fedha za kutosha kuweza kupata mtaji wa kufanya biashara katika nchi ya watu. Alipofika huko, walikubaliana kuhama katika mji huo, wakaelekea Pretoria ambako Ame alikuwa na rafiki yake aliyehamia huko miaka mingi.
Wakatafuta kazi na kupata katika supermarket moja, ambapo waliingia na kutoka kwa shift. Ame akiingia asubuhi, mpenzi wake akija jioni. Maisha yaliendelea hadi walipoamua kuacha kazi na kuanzisha mgahawa mmoja mdogo katika jengo la Mkenya mmoja ambaye walikuwa wakiitana jirani.
Maisha yaliendelea na jambo la kushukuru Mungu ni kwamba mgahawa wao ulipata umaarufu mkubwa na kuwa kituo kikubwa cha wateja kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo na hata Zambia na Malawi. Wengi walipenda kuuita mgahawa huo kwa jina la Nyumbani.
Miaka ikapita na sasa Jerry na Ame wakawa vijana maarufu sana Afrika Kusini, kwani waliongeza mtaji na kufungua migahawa mingine katika miji kama Johannesburg, Durban na Soweto na huko kote waliajiri vijana wenzao kutoka nchi za Afrika Mashariki.
**
Jijini Dar es Salaam mwaka mmoja baada ya Bata kutoka hospitalini, alikuwa bado hajapata fahamu za kutosha, kwani mara kadhaa aliweza kukumbuka shule aliyosoma au marafiki zake, lakini kumbukumbu hizo zilipotea haraka na kumrejesha alipokuwa, kitu ambacho alikichukia sana.
Siku moja Noel akiwa na mzee Masta walimchukua Bata na kwenda naye ufukweni kwa ajili ya kupunga upepo. Huko, walimnunulia soda na kumruhusu kujichanganya na vijana wenzake, aliogelea na kucheza hadi jioni walipoanza kurudi.
Wakati wakirejea, Noel akiwa kwenye usukani, walienda vizuri hadi walipofika njia panda ya Mbuyuni, wakitaka kuingia katika barabara ya Bagamoyo. Lori moja kubwa, ghafla lilionekana kupoteza mwelekeo, likalifuata gari dogo la akina Noel na kuliparamia..
Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply