The House of Favourite Newspapers

Chongo – 21

0

Ilipoishia wiki iliyopita
“Ndiyo hivyo, kitu tunachoweza kukifanya kwa sasa, ni kurudi Bongo kwa muda, maana watanitafuta sana, sasa kwa kuwa niliyemuua anajulikana sana hapa, itatusumbua, wakinikamata mimi, nyinyi hamtapona,” Sule alihitimisha mazungumzo yake na kuomba kama anaweza kupatiwa Vodka!
Sasa endelea…

“Kama unamaanisha hivyo, basi ni wazi kuwa hata sisi tunatakiwa kuondoka mara moja, maana wakikutafuta na kukukosa ni wazi kuwa watatutafuta sisi,” Jerry alisema akiifuata Vodka kwenye jokofu, wakati Mae akimtazama Sule kwa jicho la mshangao kabisa, hakuwahi kumfikiria kama angeua watu wawili ndani ya muda mfupi tangu amfahamu, akili yake ilimtuma kuamini kuwa kulikuwa na orodha ya marehemu wengi waliotokana naye.

Mwishowe wakakubaliana wote warudi nyumbani kwa muda, ili pia kama itawezekana, waifanye biashara hiyo ndani ya Tanzania. Wazo la kujishughulisha na uuzaji wa unga wakiwa Bongo halikukubalika akilini mwa Mae, ambaye alipendekeza ni vyema wakatafuta kazi nyingine halali ya kuifanya wakiwa huko kuliko hiyo.

Jerry alitangulia kufika Dar es Salaam wakati Sule alipokimbilia Mombasa kujificha kwa muda, wakati Mae alibakia Sauzi ili kuweka mambo sawa. Jerry na Mae walikubaliana kufungua ofisi ya kupokea na kusindikiza watalii katika hifadhi za taifa, biashara ambayo waliwahi kuifanya wakiwa Sauzi.

Miezi sita baadaye wote watatu wakawa wako Dar, Sule akinunuliwa teksi na kujifanya kuwa ni mfanyabiashara, lakini ukweli ni kwamba alikuwa ni mlinzi wao nyakati za usiku na mtu wa kunusa kama kuna hatari yoyote inanukia upande wao, kutoka vyanzo vyake mbalimbali.

Siku hiyo, alipompitia Mae nyumbani, alikuwa amepigiwa simu na Jerry, akiambiwa kuwepo kwa jambo muhimu la kujadili, linalopaswa kuzungumzwa wakiwa wote watatu. Walipanga wakutane katika hoteli moja tulivu wilayani Temeke, mbali na makazi yao.

“Nimepata tetesi kuwa Bata yupo hai na anatutafuta,” Jerry aliwaambia Mae na Sule baada ya kukaa na wahudumu kuwaletea vinywaji walivyoagiza, wakiwa wamejitenga katika kibanda cha peke yao.
Zilikuwa ni habari zilizoupasua vibaya mno moyo wa Mae na hivyo kumfanya kupata mshtuko mkubwa ambao Jerry aliutegemea. Sule alibakia kuwa mtulivu pale kitini alipokaa, ingawa hakumfahamu kwa sura kijana huyo, lakini alishaambiwa mkasa mzima na hivyo hakuwa mgeni nao.

Mae alipotaka kufahamu jinsi mpenzi wake alivyotambua jambo hilo, akawaambia; “Nilikuwa nimekaa na washkaji tunapiga stori sehemu, wakawa wanazungumzia suala hilo lakini bila wao kujua kama anayezungumzwa ni mimi.”

“Hiyo haitoshi bwana, hebu sema vizuri ilikuwajekuwaje?” Mae aliendelea kudai.
“Tulikuwa pale Johannesburg Hoteli tunapiga stori,katika mazungumzo jamaa mmoja akasema katika hii dunia usije ukamfanyia mtu ubaya ukadhani utakuwa salama, sasa katika kufafanua ndo akasema kuna jamaa walimpiga na kuamini wamemuua kijana mmoja hivi ili warithi mali, lakini kumbe jamaa hakufa na sasa anawatafuta,” alisema Jerry.

Mae akainamisha kichwa chake kwenye meza, mawazo mengi yakaanza kupita kichwani mwake. Jerry alilitambua jambo hilo, hivyo hakutaka kumpa nafasi ya kutafakari, alichotaka ni kijana huyo kutafutwa na kuuawa mara moja.

“Mae, lazima tuhakikishe Bata anakufa haraka, vinginevyo tutakufa sisi,” alisema huku akimtazama mwanamke huyo aliyeishi naye kwa miaka mingi sasa.
“Hapana, sidhani kama tunahitaji kumuua, tunaweza kuondoka hapa ili tumpe muda wa kuendelea na maisha yake,” alisema Mae.

“Kwani kwa mawazo yako bro, huyo Bata ni hatari kiasi gani katika maisha yako?” Sule naye alimuuliza Jerry.
“Hatari ni kubwa, kipigo nilichompa kilikuwa ni cha kumuua, nadhani unajua kisasi cha kuua ni kuua tu, kuondoka na kwenda kuishi popote duniani siyo kinga licha ya kuwa tuna uwezo huo, unajuaje kama hawezi kutufuata huko tutakapo kuwa?”
“Sidhani kama anaweza kujua tulipo, kwanza ni wachache wanaojua kama tupo Dar na hata kama ni vigumu sana kwake kujua maana siamini kama matembezi yake yanaweza kumfikisha kwenye maeneo tunapotembelea sisi,” alisema Mae.

Baada ya kubadilishana mawazo kwa muda mrefu, mwishowe wakakubaliana kuchunguza na ikiwezekana kumfahamu kijana huyo sehemu alipo, shughuli anayofanya na kama uwepo wake unaweza kuwa hatari kwa maisha yao.

Wakati watatu hao wakimaliza mazungumzo yao kwa maazimio hayo, Bata alikuwa na kikao akiwa na mpenzi wake Elina, pamoja na shemeji yake Jully, sehemu moja katikati ya Kariakoo.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo
John Kitime 0763722557

Leave A Reply