The House of Favourite Newspapers

Chongo – 29

0

Ilipoishia WIKI ILIYOPITA
“Mbona uko kimya sana, naona unazungusha kichwa tu, vipi?” Sule alimshtua mpenzi wake wakiwa wamekaa pembeni ya ua huo, wamejitenga na wengine, mwanaume huyo akinywa bia na Mwani akiendelea na kinywaji chake.
Songa nayo sasa


Hamna, naona kama dalili za homa kwa mbali ndiyo najisikilizia, halafu si nilishakuambia kuwa hii nyumba walikuwaga wanakaa washkaji zetu ambao sasa hivi wako nje?” Mwani alimwambia Sule katika namna ya kumpoteza maboya.
“Yaa nakumbuka uliniambia, sasa hiyo homa yako naona ina kisasi na mimi,” alisema huku akimpigapiga Mwani kwenye mapaja yake yaliyotulia ndani ya suruali ya kubana aliyovaa.
Hakutaka kabisa kumpoteza binti huyo siku hiyo, hivyo taarifa kwamba alikuwa akijisikia homa ilimpa presha kubwa, hata hivyo akaamua kuendelea kuwa mtulivu ili ajue mwisho wa siku nini kitatokea.
Mwani naye wala hakuwa na papara, licha ya kuwa alikuwa akiwafanyia kazi akina Bata, lakini pia hakuona ubaya kama angepoteza usiku mmoja akiwa na Sule, kwani alikuwa kijana mwenye mwili mkakamavu ambao yeye aliupenda na pia handsome na alionekana pia kutokuwa na tatizo la fedha.

Ilipofika saa tano kasorobo usiku, sehemu iliyotayarishwa ilionekana kujaa wageni waalikwa na sauti za watu pamoja na muziki sasa ziliongezeka, kitu kilichoashiria kuwa vinywaji na vitafunwa vilikuwa vinatumika ipasavyo.
“Basi ninavyowajua hawa mabosi wangu, kesho wataamka saa saba,” Sule alimwambia Mwani, akionekana kuanza kulewa, maana wakati huo kila mtu ambaye angewatazama, asingehitaji utambulisho kujua kuwa walikuwa mtu na mpenzi wake.
“Kwa nini?” Mwani alimuuliza akiwa amemuwekea miguu yake kwenye mapaja yake.
“Hawa nawajua mimi, wana vichwa vibovu ka nini, yaani kama nina shida nao wala sipati tabu ni kuwashawishi wapate ulabu tu, kila kitu kinaisha mapema,” Sule alisema bila kujua kuwa maneno yake yalikuwa yanatoa njia ya watu kufanikisha malengo yao.
Mwani akatumia muda huo pia kujaribu kuchokonoa ili kujua ni watu wangapi wanaishi ndani ya nyumba hiyo na kama yeye Sule pia alikuwa akiishi hapo. Alidodosa mambo kadha wa kadha hadi ilipofika saa saba za usiku, walipokubaliana kuondoka!
**

Bata, Ellina, Mwani na Jully walikuwa wamekaa kwenye viti pembezoni mwa bustani ya Mnazi Mmoja, wakinywa juisi ya matunda waliyonunua kutoka kwa vijana wanaozunguka viwanjani hapo. Kila mmoja aliwasilisha mrejesho wa shughuli aliyoenda kuifanya, lakini kwa siku hiyo ni wawili tu ndiyo taarifa zao zilitakiwa zaidi.
Bata alielezea kwa kirefu jinsi alivyokwenda kisha kuzungumza na Gasto, kabla ya Mwani naye kuwaeleza kwa kirefu alichokiona ndani ya nyumba wanayoishi wabaya wao, ingawa aliweka wazi pia kwamba aliondoka na kulala na Sule.
“Kwa hiyo sasa tupo na shemeji, huwezi kutuuza kweli Mwani?” Jully aliongea kwa utani, ambao ulijibiwa kuwa asingeweza kamwe kuwasaliti, kwani hata hilo penzi lenyewe lilitolewa ili lilete matunda yaliyotakiwa.
Baada ya majadiliano marefu, mwishowe wakakubaliana siku ya kufanya mashambulizi, ambayo kwa vyovyote yafanyike Sule akiwa hayupo nyumbani hapo, ikiwezekana awe amedhibitiwa na Mwani eneo f’lani mbali na walipo.

Ellina alipojaribu kutoa wazo la kuongeza watu katika shughuli hiyo, Bata alimpinga kwa kudai kuwa wao watatu wangetosha, kwani anafahamu wawili hao wasingeweza kuwaletea usumbufu, hasa kwa jinsi watakavyowaingilia!
**

Sule alikuwa anaegesha gari lake katika eneo la maegesho pale mtaa wa Samora katika jengo ambalo zimo ofisi za Jerry, wakati Bata alipomuona. Alipata mshtuko mkubwa ambao hata hivyo ni yeye peke yake ndiye aliyeuhisi. Woga wa ghafla ukampata hasa alipotambua kuwa mtu anayeteremka garini, anakwenda kuonana na mtu ambaye alitaka kutoa uhai wake miaka mingi iliyopita.
Naye alimchukulia Sule kama muuaji mwingine aliyestahili kufa sawa na Jerry. Alimtazama alipokuwa akitembea kulifuata jengo hilo na kupotelea ndani.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply