The House of Favourite Newspapers

Chongo 33

0

Ilipoishia wiki iliyopita
Mwani alitoka nje, mkono wake mmoja ukiwa umeshikilia sehemu ya katikati ya paji lake la uso, kitambaa chake cha mkononi kikiwa kimeloa damu!
Sasa endelea…

Juddy alishtuka kuona damu, akili yake ilifikiria matukio mengi ndani ya sekunde chache kabla ya kukataa kujiumiza kuwaza wakati angeweza kujua kilichotokea kutoka kwa mhusika aliyesimama mbele yake.
“Umekuaje tena Mwani?” Juddy aliuliza kwa wasiwasi. Lakini tofauti na matarajio yake, Mwani hata hakuonesha wasiwasi, alisonya wakati akifuta vizuri damu hiyo kwa kitambaa na baadaye akamweleza kuwa aliumia baada ya kujigonga kwenye kuta za chemba wakati akirejea.
Wakarudishia vizuri mfuniko wa chemba hiyo, kisha wakaondoka kwa tahadhari hadi nyumbani kwao, wakakaa sebuleni wakijifanya kuangalia televisheni kidogo ili kuwapumbaza wazazi kama wataanza kuwafuatilia. Walipoona kila mtu ana shughuli zake, wakaingia chumbani kwao na kujirusha kitandani.

“Nhee, lete mchapo, maana naona kazi imeanza,” Juddy alimwambia Mwani.

“Kazi ni nyepesi kuliko nilivyokuwa nafikiria aisee, akipatikana mtu wa bunduki, ni wanapigwa kutokea ndani ya chemba, hatuna hata haja ya kuwafuata,” Mwani alimweleza mwenzake kila kitu kwa jinsi alivyoona kutoka pale alipokuwa.
Usiku uleule, wakawapigia simu akina Bata na kuwaeleza hatua aliyokuwa amefikia usiku ule, wakakubaliana wakutane kesho yake mapema ili waweze kupanga mambo yao, kwani siku zinazidi kukimbia.

Saa tano asubuhi, Bata, Jully, Mwani na Ellina walikuwa wamekaa kwenye meza moja, katika klabu ya Jeshi ya Msasani Beach, Kawe jikoni wakiwa wameagiza supu ya samaki iliyokuwa na wateja wengi. Waliamua kukutana eneo hilo wakiamini ni salama kwao.

Mwani aliwaeleza vijana wenzake mazingira yote yalivyokuwa ndani ya chemba na jinsi ambavyo mtu mwenye bunduki anaweza kuwaua wanandoa hao kutokea shimoni, kwani Jerry na mkewe walionekana kuwa na tabia ya kupenda kukaa kwenye makochi yaliyopangwa kwenye kibaraza cha nje ya nyumba.

“Jamani, kwa hiyo mnataka kuniambia hawa jamaa wafe tu bila kuonja mateso kama Bata alivyofanyiwa?” Ellina aliwauliza wenzake huku akimtazama mpenzi wake aliyekuwa akitoa tabasamu.

“Suala la aina ya kifo au mateso lipo mikononi mwa Bata, karibu utupe mipango,” Mwani alisema huku akiizima simu yake, maana Sule alikuwa akimpigia kwa mara ya kumi ndani ya dakika mbili.

“Kiukweli, mimi sitaki tuwaue, ila nataka wapate adhabu ambayo wataiutia katika maisha yao yote yaliyobaki, kuua siyo namna ya kumpa adui yako maumivu,” alisema Bata na kuwafanya wasichana watatu waliokuwa mbele yake kumshangaa.
“Katika kosa kubwa ambalo hupaswi kulifanya ni kuwadhuru na kuwaacha hai hao jamaa, wewe mwenyewe ni mfano halisi wa jinsi gani wanaweza kuja kivingine na kukuangamiza. Kama wangejua wewe uko hai, nina imani kabisa wangekuwa hawana amani ndani ya mioyo yao, lakini kwa kuwa wanajua ulishakufa, ndiyo maana wanajiachia,” Jully alisema.

Ukafuata mjadala mkubwa, lakini kwa sauti za chini kabisa kiasi kwamba mtu aliyekuwa meza inayofuata, asingeweza kuelewa kilichoendelea. Wakaweka mpango huu, wakabadili, wakaujenga huu, wakaufuta na mwishowe, wakakubaliana…
***
Sule hakuamini macho yake baada ya msichana mmoja mrembo, mwenye asili ya Kiarabu alipovuta kiti na kukaa katika meza yao. Haraka alipomkisia umri, hakuwa amefikisha hata miaka ishirini.
“Twaha mambo?” msichana huyo alisabahi huku akimtazama zaidi Sule. Twaha akaitikia kisha akamwambia Sule.

“Mgeni wetu huyu kaka, karibu Monny.”
Sule alikuwa ametembea katika nchi nyingi na kuona warembo wengi, lakini msichana aliyekuwa amekaa pembeni yake, alimkumbusha wasichana wazuri aliowahi kuwaona katika Ufukwe wa Copa Cabana kule Brazil. Alikuwa mkali hasa.
Sule akamshika mkono kusalimiana, baadaye wakaungana katika kinywaji na mazungumzo. Kwa mshangao wake Sule, Monny alimwambia hanywi pombe, zaidi ya maji ya matunda na vyakula.

“Mimi mtu wa misosi bwana, aitwe kijana wa jikoni nifanye yangu,” Monny alisema huku akichekacheka. Alijiagizia alivyotaka na kuletewa, huku vijana wale wawili wakiendelea kunywa bia.

“Nheee nimekumbuka Sule, yule dogo kumbe anaishi hukuhuku Sinza, mshkaji kaniambia, tena mitaa hiihii ya karibu, ni kati ya hapa Palestina hadi Kwa Remmy,” Twaha alitoa kauli iliyomshtua sana Sule hadi kila mmoja akajua kuwa ameshtuka.

“Weeeee, kumbe nipo jirani kabisa na shujaa ninayemzimia?” Sule alijilazimisha kutabasamu na kujiweka katika hali yake ya kawaida. Alikuwa amechelewa, mshtuko wake uliwapa wasiwasi mkubwa Twaha na Monny, lakini hawakutaka kuonesha lolote. Hata hivyo, msichana huyo hakuelewa nani alikuwa anazungumziwa.

Mwili wa Sule ukafa ganzi, mshtuko wake ulimshtua hadi yeye mwenyewe. Akajiona mjinga kuweza kuwaonesha mshtuko wake na ili kuimaliza ishu hiyo, akaamua kutozungumza lolote kuhusu Bata kwa siku ile.

Saa kumi na moja hivi, kinywaji kikiwa kimekolea, Sule alimtaka Monny waondoke zao. Binti hakupinga, wakainuka pamoja, wakaingia garini huku Twaha akiwasindikiza kwa macho. Gari likageuka, likanyoosha hadi barabarani, likapinda kushoto na pale Makaburini, wakaifuata njia ya kuelekea barabara ya Sam Nujoma.

“Hivi pale mlikuwa mnamzungumzia nani hadi ukashtuka namna ile?” Monny, akiwa ndani ya kanga moja, katika nyumba moja ya kulala wageni, The Place House, alimuuliza Sule, ambaye mkononi alikuwa na bia yake ya kopo.
Alishasahau, akarudisha nyuma akili zake akakumbuka ile ishu ya Bata. Kwa kuwa hakuwa akimjua msichana huyo na wala hakujua kichwani mwake mna nini, akamsimulia mkasa wa kushangaza wa kijana huyo.

“Namjua, hadi nyumba anayokaa naijua, jina lake anaitwa Bata, mtanashati sana yule mkaka, ila simulizi yake ndiyo inasikitisha, ila jamani yuko poa sana,” Monny alisema huku akimpetipeti Sule, mahaba yakiwa wazi machoni mwake.
Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply