The House of Favourite Newspapers

Chongo!-4

1

Ilipoishia wiki iliyopita

“Ame, kuna jambo moja muhimu nataka kukuambia, kukubali au kukataa kwako kutakuwa na maana mbili, kuharibu au kuboresha uhusiano wetu,” alisema huku akimtazama Ame, aliyeshtusha na maneno hayo.

Sasa endelea…A

me alimtazama bila kujua mpenziwe alikuwa na maana gani, akaendelea kubaki kimya ili asikilize kitu gani ataambiwa. Jerry akakohoa, ishara kwamba alitaka kuendelea.

“Nina wazo moja, maisha yetu mazuri yanaweza kugeuka karaha kama hatutajipanga tangu mwanzo kukomesha hatari yoyote tunayodhani inaweza kuja. Niwe mkweli, mdogo wako Bata namuona kama mtu atakayetunyima raha za maisha,” Jerry alimweleza mpenzi wake ambaye alishtuka na kuuliza haraka.

“Kivipi, mbona sikuelewi Jerry,”

“Nisikilize unielewe, unajua Bata bado kijana mdogo, sisi ndiyo tutakaofanya kazi kubwa kuimarisha na kuendeleza miradi ya mzee wenu, atakapokuja kuwa mkubwa, hatanithamini mimi, ataweza hata kuniondoa bila chochote,” alisema Jerry, uso wake ukimaanisha alichokuwa akiongea.

“Bado sikusomi, nakuona kama unazungukazunguka, akuondoe bila chochote kivipi, kwani wewe si unaoana na mimi, Bata anaingiaje?” Ame, naye uso ukiwa ameukunja, alisema.

Baada ya huku na kule, hatimaye Ame akamuelewa mpenzi wake. Jerry alitaka Bata auawe, ili yeye na mpenziwe wawe ndiyo wamiliki pekee wa mali iliyoachwa na marehemu baba yao, akiamini kuwa wataiendeleza kama yao na hivyo kuyafurahia maisha yao.

“Hilo ni jambo kubwa na gumu sana Jerry, ninakupenda lakini sioni ni vipi ninaweza kukubali hilo, tunaweza kufurahia maisha kivyetu na Bata akawepo kivyake, kwani sisi si tutatafuta hela zetu? Achana na hayo mawazo bwana, huyu tunaweza kumdhibiti na kila kitu kikawa sawa,” alisema Ame, akimtazama kwa mshangao Jerry.

Kwa kuwa alishasema, Jerry aliiona hatari ya kukubali kirahisi kushindwa, akatumia mifano, hadaa na vishawishi chungu nzima hadi Ame akakubaliana naye, akaruhusu kifo kwa mdogo wake, lakini kwa masharti kuwa kitendo hicho akifanye Jerry mwenyewe.

“Hii ni siri, tunazungumza wawili na jambo hili lazima ulifanye wewe mwenyewe kwa mikono yako. Usimtume mtu ili siku ukija kunigeuka huko mbele ya safari, damu yetu iwe mikononi mwako.”

Hilo lisingekuwa tatizo kubwa kwa Jerry, kwa sababu tangu awali asingeweza kumpa mtu kazi hiyo kwa kuhofia usalama wake siku za mbele.

***

Bata alikuwa mmoja kati ya vijana waliokuwa wakipenda sana kucheza mpira wa miguu mtaani kwao na tena alikuwa ana kipaji kikubwa sana. Kila mmoja alimtabiria kufika mbali katika soka na kwa umri wake wa miaka kumi tu, tayari alikuwa na majina mengi ya utani.

Mtaani kwao, Bunju jijini Dar es Salaam alijulikana kama Messi, wakati shuleni kwao, walimwita Ronaldo. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira na vile alikuwa akisoma shule ya binafsi, wengi waliamini atapata elimu bora, hivyo uhakika wa kucheza mpira Ulaya ulikuwa ni mkubwa.

Uwezo wake ulimfanya mara kadhaa kufanya mazoezi na timu za watoto waliomzidi umri, kwani kwa wenzake alionekana kama anawaonea. Siku hiyo alikuwa ametoka kushiriki katika mechi ya watoto wa mtaani kwao, waliokuwa wameenda kucheza huko Nakasagwe, jirani na Bunju.

Basi dogo walilokodi lilikatiza mitaa, likapitia katika gereza la Boko, kabla ya kuingia barabarani na mwendo mchache baadaye, likaegeshwa nje ya uwanja wa shule. Wakiwa wameshinda mchezo huo, waliteremka huku wakiimba, kila mmoja akielekea nyumbani kwao.

Bata, ambaye nyumba yao ilikuwa umbali kidogo kutoka eneo la shule, alitembea bila wasiwasi kwani giza la saa moja usiku hakulitilia shaka. Ili kufika nyumbani kwao, alilazimika kuzipita nyumba mbili zilizokuwa bado zinajengwa zilizopeana migongo, kila siku alikuwa akipita njia hiyo.

Alipoanza kuipita nyumba ya kwanza, nywele zake zikasimama na mwili ukamsisimka. Akapatwa na woga wa ghafla akataka kupiga kelele lakini kabla hajafanya chochote, mbele yake akatokea Jerry!

Hofu ya Bata ikapungua. Alikuwa anamfahamu shemeji yake, mpenzi wa dada yake Ame. Wakati anajiandaa kumsalimia, kitu kisicho cha kawaida kwake kikatokea!

1 Comment
  1. masau magesa says

    Namkubali sana mtunzi, ananigusa sana

Leave A Reply