The House of Favourite Newspapers

Chongo!-7

0

Ilipoishia wiki iliyopita

“Hebu piga simu mapokezi, walete machela haraka, kuna uhai kwa mbali kwa huyu kijana, huenda Mungu bado hajaamua,” alisema daktari huyo huku akimlegeza baadhi ya nguo alizofungwa Bata.

Sasa endelea…

N

oel na mzee Masta wakapigwa na butwaa, tangu mwanzo hawakuwa na wazo kama kijana huyo angeweza kuwa mzima. Nao wakatoa macho kwa mtu wa mochwari, yenye kuonyesha msisitizo wa kuitwa haraka kwa watu wa mapokezi.

Sekunde chache baadaye machela ikaletwa, wakampakiza na haraka akakimbizwa katika chumba cha upasuaji ambako Noel na mzee Masta hawakutakiwa kuingia. Baada ya kubaini hivyo, nao wakageuza kuelekea polisi, ambako waliwataarifu juu ya kilichoendelea.

Baada ya kutoa maelezo hayo polisi, walirejea tena hospitalini na kuulizia kinachoendelea. Walijikuta wakikumbatiana kwa furaha baada ya kuambiwa kuwa kijana huyo bado ni mzima, ila ana hali mbaya sana na kupona kwake ni majaaliwa ya Mungu tu.

Kwao, huo ulikuwa ni sawa na ushindi, maana kwa hali aliyokuwa nayo, akiwa hajitingishi kwa muda wote tangu alipotupwa hadi anaokotwa, halikuwa jambo la kutegemewa hata kidogo. Wakaambiwa kuwa bado amepoteza fahamu na muda mchache ambao wangeweza kukadiria kurudiwa na fahamu, basi baada ya saa 72, sawa na siku tatu!

Walipoambiwa hivyo, wakaomba angalau wakamuone pale alipolala kitandani, wakakataliwa. Kwa masikitiko makubwa wakaondoka na nje, Noel akampeleka mzee Masta stendi ya magari ili akapate usafiri arudi kijijini Makaani, kwa makubaliano kuwa siku ya tatu wakutane hapo ili waende wakamuone mgonjwa, ambaye alishakuwa wao maana majina yao yaliandikwa kwenye vitabu vya kumbukumbu.

***

Jerry na Ame walikuwa wamekaa kwenye bembea, katika ufukwe wa Bahari ya Hindi wakiwa na soda zao za kwenye kopo katika mgahawa wa Coco Cabana, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Jerry alikuwa mwenye furaha, lakini Ame hakuwa na raha hata kidogo, moyo wake ulimtesa sana alipomfikiria marehemu mdogo wake, Bata.

“Siku zote maisha mazuri huja kwa kujitoa, usiogope wala kufikiria sana, wapo wengine huua familia nzima, hata wawe kumi, sembuse wewe mmoja tu,” Jerry alimtuliza Ame, ambaye badala ya kujibu, aligeuka kumtazama huku akinywa soda yake kama anayelazimishwa.

“Hivi unafikiri ndugu zangu nitawaambia nini mimi, hadi leo sijasema lolote maana sijui la kuwaambia,” Ame alimwambia mpenzi wake akiwa bado na uso mtulivu uliokosa amani.

“Tukae huku siku tatu, tutakaporudi ndipo utaanza kuwaulizia ndugu zako kama wanajua alipo maana utasema ulipoondoka ulimuacha nyumbani lakini hujamkuta,” Jerry alimwambia mpenzi wake, moyoni mwake akiwa na furaha isiyo kifani.

“Hivyo una maana hata kaburi lake sitaliona, ni haki kweli hiyo Jerry,” msichana huyo alimwuliza mwenzake.

“Hatuna jinsi, kwa sababu kama tutajaribu kuonyesha kuwa tumemwona sehemu, lazima tutahojiwa sana na mwishoni tunaweza kubainika, cha kufanya baada ya wiki mbili twende kule tulikomtupa, tunaweza kupata fununu ya wapi mwili ule ulipelekwa.”

“Basi tu yaani, lakini hii yote nafanya kwa ajili ya mapenzi yako, sidhani kama wewe ungeweza, Mungu anajua kila kitu kitakavyokuwa,” Ame alisema akionyesha wazi majuto yake.

Walikaa Zanzibar kwa siku tatu zaidi na siku hiyo asubuhi na mapema, walikuwa bandarini ambako walipanda boti ya saa tatu asubuhi, wakitarajiwa kuwasili Dar es Salaam majira ya saa nne na nusu. Njiani, walikuwa kimya wakiangalia televisheni iliyokuwa ikionyesha matukio mbalimbali ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

***

Noel akiwa na mkewe, alifika mapema stendi ya mabasi pale Bagamoyo, alipowasiliana na mzee Masta, akamwambia alikuwa njiani na angetumia kama dakika kumi kutokea muda huo kuwasili hapo. Noel akasogea katika mgahawa mmoja, akaagiza maziwa ya moto akimsubiri.

Alipowasili, wakaingia ndani ya gari na moja kwa moja hadi hospitalini, ambako waliongozana moja kwa moja hadi chumba cha upasuaji. Wakaulizia kwa nesi waliyemkuta kuhusu maendeleo ya mgonjwa wao.

“Yukoje?” dada huyo aliwauliza akiwa mtulivu pale kwenye meza yake iliyo nje ya chumba hicho.

“Ni kijana tu, yapata umri kama miaka kumi au kumi na mbili, tulimleta juzi,” alisema mzee Masta akimtazama kwa makini usoni msichana huyo.

“Hatuna mgonjwa kama huyo, humu ndani kuna majeruhi wanne tu, tena wote watu wazima, wanawake wawili na wanaume wawili, wamepata ajali ya gari leo asubuhi,” alisema msichana wa mapokezi.

Ni kweli Bata hayupo? Nini kimemtokea? Usikose kupata majibu ya maswali haya katika toleo lijalo.

Leave A Reply