Chongo-7
Ilipoishia wiki iliyopita
Noel na Mzee Masta wakaanza kusogea taratibu, wakaona kama mtu aliyefunikwa shuka, wakasogelea na kubaini kuwa alikuwa ni mtu, lakini kijana mdogo. Ni Bata.
Sasa endelea…
Damu zilikuwa zinavuja maeneo mbalimbali ya mwili wake. Kwa jinsi walivyomuangalia, walishindwa kujua kama amekufa au yu hai.
Bila kuambizana, wakambeba, wakamwingiza kwenye gari, wakamlaza kiti cha nyuma, wakaondoa gari hadi barabarani, wakakubaliana kumuacha mkewe Noel, ili mzee Masta aongozane na Noel kuelekea polisi.
Gari liliondoka taratibu kuifuata njia ya Bagamoyo, wote wawili walikuwa na wasiwasi mkubwa na majeruhi waliyempakia nyuma ya gari, hawakuelewa tatizo hasa lilikuwa ni nini. Kabla hawajafika njia panda ya barabara ya Msata, Noel akasimamisha gari.
“Mzee Masta, unaonaje tumchunguze mtu tuliyembeba? Tujue nini kinaweza kuwa kimemsibu, maana huko tunakoenda tuwe angalau na cha kuanza kuzungumza,” Noel alimwambia mzee Masta, wakakubaliana. Wakafungua milango na kutoka nje, wakamfunua mtu waliyembeba.
Walipomchunguza, bila kuhitaji ushahidi zaidi, wakajiaminisha kuwa kijana mdogo aliyempakia, alikuwa amepigwa, tena vibaya na uwezekano wa kuwa mzima, ulikuwa ni chini ya asilimia tano. Wakaendesha gari hadi Kituo cha Polisi Bagamoyo.
“Tuna kijana kwenye gari, tumemuokota, anaonekana amepigwa na kutupwa porini, hatujui kama yu hai au amefariki,” mzee Masta alizungumza mbele ya kaunta ya polisi, huku Noel akiwa pembeni yake, akichezea funguo za gari lake.
“Wewe ni nani na jambo hilo limetokea wapi, ilikuwaje kuwaje,” askari aliyekuwa kaunta alimuuliza, huku akimwamuru mwenzake aliyemuita kwa cheo cha dokta, kwenda kuangalia kilichomo kwenye gari.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Makaani, nilikuwa namuonesha huyu kijana sehemu ya shamba lake, sasa wakati wa kurudi ndipo tukamuona huyo kijana ametupwa, tukamchukua,” alisema mzee Masta, uso wake ukiwa hauna chembe ya hofu, licha ya askari huyo kumtazama machoni kwa muda wote.
“Afande, nadhani ni maiti tayari, waipeleke kwanza chumba cha maiti hospitalini kisha warudi kwa maelezo zaidi,” yule askari aliyeambiwa kwenda kuangalia majeruhi ndani ya gari alisema, jambo lililowaumiza sana Noel na mzee Masta.
Wakawasha gari hadi Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, mzee Masta alifahamu eneo kilipo chumba cha maiti. Wakasimamisha gari nje ya ofisi na kuteremka.
“Tumeleta mwili huu wa kijana tumemuokota huko shambani,” alisema mzee Masta huku akimpatia mfanyakazi huyo wa chumba cha maiti karatasi maalum kutoka polisi. Akaipokea, akaitazama na baadaye akawaambia wauteremshe mwili ili waupeleke chumbani.
***
Jerry na Ame walirejea nyumbani wakiwa wamechoka mno, hasa msichana huyo ambaye moyo wake ulimsuta sana kwa kitendo alichomfanyia ndugu yake. Hata hivyo, alijisikia faraja kwamba mtu aliyempenda kuliko wanaume wote duniani, alikuwa na furaha naye.
Walifika hadi nyumbani kwa akina Ame. Nje kabla ya kuingia ndani, Jerry akamwuliza mchumba wake ni kitu gani watawaeleza ndugu zao endapo watauliza kuhusu wapi alipo Bata. Baada ya majadiliano ya kama dakika kumi hivi, hatimaye wakakubaliana kwamba endapo Ame ataulizwa, aseme hafahamu alipo.
Lakini ili kusogeza mbele siku, wakakubaliana kusafiri siku inayofuata kwa ajili ya kwenda kupumzika na kutuliza akili Zanzibar. Wakabusiana, Ame akaliingiza gari ndani na Jerry akashuka na kuchukua teksi kuelekea nyumbani kwake. Kesho yake asubuhi, walikuwa Ferry, wakichukua tiketi za boti na saa tatu kamili, safari ya kuelekea kisiwani ikaanza!
***
“Sasa wazee, kwa mujibu wa taratibu, tunatakiwa tusubiri kidogo ili daktari aje kuthibitisha kama huyu kijana amefariki kweli. Ni suala la utaratibu nadhani hata dakika tano hazichukui,” mfanyakazi wa chumba cha maiti aliwaambia mzee Masta na Noel ambao walishaanza kujiandaa kuondoka.
Mfanyakazi huyo akaenda mezani kwake na kuzungusha namba kadhaa kupitia simu ya mezani, akazungumza na mtu akimfahamisha kuwa alihitaji daktari wa kuja kuthibitisha kifo kabla maiti haijawekwa chumbani. Wakiwa wamesimama nje ya chumba, dakika tano baadaye daktari mmoja aliingia chumbani, nao wakaingia pamoja naye.
Akiwa amechomeka masikioni vipimo vyake, alivitoa na kuviweka kwenye eneo la moyo la mwili wa Bata na kusikiliza. Ilimchukua sekunde kadhaa kabla ya kuitoa na kuirejesha tena eneo lilelile, baadaye akahamisha katika maeneo kadhaa ya mwili ule.
“Hebu piga simu mapokezi, walete machela haraka, ana uhai kwa mbali kwa huyu kijana, huenda Mungu bado hajaamua,” alisema daktari huyo huku akimlegeza baadhi ya nguo alizofungwa Bata.
Je, nini kitatokea? Bata atapona? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo
JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!