Chris Mugalu Mchezaji Bora
MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba , Chris Mugalu amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Julai wa Ligi Kuu (VPL), msimu wa 2020/21, huku kocha Nasreddine Nabi wa Yanga akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Mugalu alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake mwezi Julai na kuonesha kiwango cha kuvutia akifunga mabao matano, Simba ikichezw michezo mitano ikishinda mitatu, sare moja na kupoteza mmoja.
Wengine walioingia fainali ni Charles Ilamfya wa KMC na Juma Liuzio wa Mbeya City waliozisaidia timu zao kwa namna moja ama nyingine. Kwa mwezi Julai Simba ilizifunga Coastal Union 2-0, Namungo 4- 0 na KMC 0-2, kisha kutoka 1-1 na Azam na kufungwa 0-1 na Young Africans SC.
Kwa upande wa Nabi aliiogoza Yanga kushinda michezo mwili na kutoka sare mmoja ikiifunga Simba mabao 0-1, Ihefu mabao 2-0 na kutoka 0-0 na Dodoma Jiji, amewashinda Didier Gomes wa Simba na Mathias Lulle wa Mbeya City.
Wachezaji ambao wametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi kwa msimu huu ni Prince Dube (Septemba), Mukoko Tonombe wa Yanga (Oktoba), John Bocco wa Simba (Novemba), Saido Ntibazonkiza wa Yanga (Disemba).
Wengine ni Deogratius Mafie wa Biashara (Januari), Anuary Jabir wa Dodoma Jiji (Februari), Luis Miquissone wa Simba (Machi), Clatous Chama wa Simba (Aprili), Prince Dube wa Azam (Mei) na John Bocco wa Simba (Juni).
Makocha waliotwaa tuzo hiyo ni Aristica Cioaba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedric Kaze aliyekuwa Yanga (Oktoba), Charles Mkwassa wa Ruvu Shooting (Novemba), Cedrick Kaze aliyekuwa Yanga (Disemba).
Wengine ni Francis Baraza aliyekuwa Biashara (Januari), Zuberi Katwila wa Ihefu (Februari), Mohammed Badru aliyekuwa Gwambina (Machi), Didier Gomes wa Simba (Aprili), George Lwandamina wa Azam (Mei) na Didier Gomes wa Simba (Juni).
Wakati huohuo, Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Sokoine Mbeya, Modestus Mwaluka, kuwa mshindi wa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Julai.
Ushindi wa Meneja huyo umefuatia kufanya kwake vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo iliyofanyika kwenye uwanja huo kwa Juni pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.