Chuji, Tegete wapo sokoni Mwadui
Khadija Mngwai,
Dar es Salaam
WACHEZAJI wa timu ya Mwadui FC ya mkoani Shinyanga, wamejikuta wakiingia sokoni kufuatia mikataba yao kumalizika mwishoni mwa msimu huu ambapo kwa mujibu wa sheria za usajili za soka, mchezaji anakuwa huru akiwa amebakiza miezi sita.
Mwadui ipo katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 15 nyuma ya Stand United yenye pointi 16 ambayo lengo lake ni kumaliza katika nafasi ya nne.
Akizungumza na Championi Jumatano, kocha msaidizi wa timu hiyo, Habibu Kondo, amefunguka kwa kusema kuwa, wachezaji wao wote kwa sasa wapo huru ambapo wanaweza kuzungumza na timu yoyote.
“Wachezaji wote wa Mwadui walisaini mikataba ya mwaka mmoja kila mmoja, hivyo kwa sasa ni wachezaji huru na wanaweza kuongea na timu yoyote kwa mujibu wa sheria ambapo wanaruhusiwa kuzungumza na timu nyingine wakiwa wamebakiza miezi sita.
“Kwa upande wetu hatuna mpango wa kumuacha mchezaji yeyote labda ikitokea mchezaji ameamua kuondoka mwenyewe kwa kupata timu nyingine, hatutakuwa na jinsi.
“Kikosi chetu kipo vizuri na wachezaji wote tumewapa mapumziko ya wiki mbili na watarejea kuanza mazoezi Novemba 15 kwa ajili ya kumalizia michezo iliyobaki ya mzunguko wa kwanza,” alisema Kondo.