
NI Ijumaa nyingine tunapokutana jamvini, nakukaribisha kwa moyo mkunjufu. Wiki iliyopita tulianza kujadiliana kuhusu mada hii, ya kuwa makini na mambo ya kuzungumza unapokuwa na mwenzi wako. Leo tunaendelea kuanzia pale tulipoishia:
Zipo mada nyingi ambazo unaweza kuzungumza na mwenzi wako, na wote mkafurahi bila kukwazana wala kumfanya ajisikie vibaya. Zifuatazo ni mada mbalimbali unazoweza kuzungumza na mwenzako na akajisikia furaha kuwa na wewe, bila kujali mmekaa pamoja kwenye uhusiano kwa muda gani. Hata kama mtakaa siku nzima, hatakuchoka na atatamani muendelee kukaa karibu.
Tunajua kwamba kutoana out hasa mwishoni mwa wiki ni jambo linaloimarisha sana mapenzi. Hebu muulize mpenzi wako, mtakapotoka kwa mara nyingine anataka muende sehemu gani ambayo ataifurahia.
Hata kama ndiyo kwanza Jumatatu na wikiendi ipo mbali, muulize tu kisha msikilize atakavyokujibu. Pangeni pamoja siku hiyo itakavyokuwa na hiyo itawasaidia nyote wawili kuimaliza wiki kwa shauku kubwa ya kuisubiri siku husika. Hatachoka kukusikiliza na hakikisha unatimiza ahadi hata kama ni kwa kiwango kidogo.
Muoneshe kwamba ana mambo mengi yanayokufurahisha. Mkumbushe mambo aliyokufanyia siku za karibuni ambayo bado unayakumbuka na kuyafurahia. Utamfanya ajisikie furaha ndani ya moyo wake na atakuwa na hamu ya kukusikiliza na kukufanyia mengine mazuri zaidi. Hata kama alikununulia soksi au kitambaa cha mkononi, mueleze jinsi ulivyokifurahia.
Muulize kuhusu vitu anavyoviogopa au vinavyomfanya akose amani (hasa wanawake). Hata kama akikwambia vitu vidogovidogo, mfano anamuogopa mbwa wa jirani kwani huwa anamtishia kila siku akipita, au anaogopa mende waliopo kwenye kabati lake la nguo, moyoni atafurahi kwa sababu atajua yupo mtu anayemjali na ambaye yupo tayari kumlinda.
Zungumzieni kuhusu kazi. Kama nyote mmeajiriwa, anza kwa kumueleza mambo yanayokukera kazini kwenu, mfano ukali wa bosi wako au umbali kisha utamsikia na yeye akizungumza yake. Kama mmoja wenu hafanyi kazi, jenga mazoea ya kumsimulia jinsi siku yako ilivyokuwa ukiwa kazini au nyumbani. Itamfanya ajihisi ana umuhimu mkubwa kwako.
Msimulie ndoto za maisha yako, labda kwa mfano unapenda kufikia wapi baada ya mwaka mmoja, miwili au mitano ukiwa naye. Hiyo itamjenga na kumuaminisha kwamba kumbe atakua na maisha marefu na wewe, jambo litakalozidi kumfanya akupende.
Epuka kuzungumzia mapungufu yake, hata kama unajua anayo. Huwezi kumwambia mwenzi wako moja kwa moja kwamba mapenzi anayokupa hayakufikishi pale unapopataka. Zipo namna za kumfikishia ujumbe lakini si kwa maneno makavu.
Huwezi kumwambia mwenzi wako kwamba siku hizi amezeeka, hana mvuto tena kama zamani, au amenenepea, ile shepu yake iliyokufanya umpende haipo tena, hata kama unachokisema ni kweli.
Unapozungumza naye kwa maneno makavu namna hii, unamfanya ajisikie vibaya sana ndani ya moyo wake na huwezi amini, kauli zako zitakuwa zinajirudiarudia ndani ya kichwa chake kwa muda mrefu na atapoteza furaha anapokuwa na wewe. Zipo mbinu za kumfikishia ujumbe bila kumfanya aumie moyoni mwake.
Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

