The House of Favourite Newspapers

Chunga Sana Damu Changa Bongo Fleva 2017

rayvannyMakala: Andrew Carlos, Gazeti la Ijumaa Wikienda, Toleo la Januari 2, 2017

IKIWA imepita siku moja tangu tuanze Mwaka 2017 katika tasnia ya burudani hususan kwenye Muziki wa Bongo Fleva, wapo wanamuziki chipukizi (damu changa) ambao wamefanya vizuri kwa Mwaka 2016.

Japo kuna damu changa ambazo ziliunganisha toka mwaka juzi, pia zimeungana na za mwaka jana na kuonesha kuwa zitakuwa tishio kwa mwaka huu na katika makala haya yanawachambua zaidi;

galatoneGalatone

Alianza kuibuka 2015 akiwa na Ngoma ya Sina Mali ambayo haikufanya poa sana lakini mwaka jana alitikisa vilivyo kwenye chati mbalimbali za redio na sehemu za starehe akiwa na Ngoma ya Samaki iliyochezewa mikono na Prodyuza Dunga.

Licha ya kuendelea kutoa ngoma nyingi nzuri baada ya Samaki kama vile Shilingi, Galatone anasimama kama mmoja kati ya wasanii damu changa wanaotarajiwa kufanya makubwa Mwaka 2017 kutokana na kuimudu sauti yake vizuri.

baraka-prince-2

Barakah  The Prince

Tangu alipoibuka na Ngoma ya Siachani Nawe miaka miwili iliyopita, Barakah ameonesha si msanii wa kushuka kiwango. Licha ya kuwa na skendo za hapa na pale ikiwemo ya kudanganya mjengo, msanii huyu anabaki kuwa moja ya vipaji adimu kwenye Bongo Fleva akiwa na ngoma zake kadhaa kama Siwezi na Nisamehe aliomshirikisha Ali Kiba ambazo amezitendea haki.

Anatarajiwa kutikisa tena mwaka huu kutokana na kuwepo katika lebo ya uhakika ya Rockstar4000 ambayo inasimamia kazi zake akiwa sambamba na Lady Jaydee na Ali Kiba.

rayvanyRayvan

Ni moja kati ya zao kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) akiwa sambamba na Harmonize, Rich Mavoko na Queen Darleen. Rayvan ama Raymond ambaye anamilikiwa na Diamond katika lebo hiyo, amekuwa na mafanikio makubwa kwa Mwaka 2016 baada ya kuibuka na vibao vikali vilivyotikisa kwenye tuzo na chati mbalimbali kama vile Kwetu, Natafuta Kiki na Salome alioshirikishwa na Diamond.

Uwezo wa sauti na kutunga mashairi unamfanya kuwa mmoja kati ya damu changa za kuchungwa kwa mwaka huu wa 2017.

nandyNandy

Ukiondoa Mwasiti, Linah, Alice na Recho wanaokubalika kwa sasa, Nandy anasimama kama mmoja kati ya wasanii wa kike waliokuja kwa kasi kutoka Jumba la Vipaji (THT).

Alianza kubamba na Ngoma ya Bye Bye My Ex kisha akafanya Cover ya Mwasiti, Nalivua Pendo na mwisho akamaliza na Ngoma ya Gusagusa akimshirikisha Mr Blue.

Nandy anayefahamika pia kwa jina la Faustina Mfinanga, mwaka jana ulikuwa wa mafanikio zaidi baada ya kuiwakilisha vyema Tanzania kwenye shindano la kuimba Afrika lililofanyika nchini Nigeria la Tecno Own The Stage na kuambulia nafasi ya pili.

Licha ya kuwa nguzo ya THT katika kuimba ‘back vocal’, Nandy anatarajiwa kuwa damu changa tishio kwa mwaka huu.

malaika77Malaika

Miaka mitatu nyuma alikuwa akiwaremba wasanii kabla ya kufanya video pale Visual Lab kwa Adam Juma. Aliachana na hayo na kuibuka na Ngoma ya Mwantumu kisha Sare Sare ambazo zilimuweka kwenye ramani ya Muziki wa Bongo Fleva.

Mwaka jana aliendelea kuburuza baada ya kuibuka na Ngoma ya Rarua ambayo imempa mashavu ya kupiga shoo nyingi zikiwemo nchini Marekani.

Anaendelea kutazamiwa pia mwaka huu kama damu changa ya kuchungwa kutokana na kila anapoibuka na ngoma huwa gumzo.

ivrah

Ivrah

Ukipenda waweza muita Hamis Hamidu au Double H ila wengi wamemfahamu mwaka jana kwa jina la Ivrah.

Ivrah ni mmoja kati ya wakali kutoka Jumba la Vipaji (THT) ambapo mwaka jana alisumbua kwenye chati mbalimbali na Ngoma ya Shusha inayoendelea kufanya vizuri hadi sasa.

Kutokana na uwezo wa kucheza na sauti, Ivrah anatazamiwa kuwa moja kati ya damu changa za kuangaliwa zaidi mwaka huu.

foby

Foby

Kwa mara ya kwanza, Foby alianza kujulikana katika ‘Project’ iliyoitwa Bwelakuni ambayo iliwajumuisha wasanii wa Ruvuma iliyofanyika katika Studio za C9 Kanjenje.

Katika project hiyo, Foby alisimama kwenye kiitikio na kuonesha ubora kiasi cha kumvutia mmiliki wa studio hiyo na kufanya naye ngoma ya peke yake ya Star.

Ngoma hii ya Star inabaki kuwa moja na ngoma zilizomuwezesha kujulikana na wengi kiasi cha kupata ‘interview’ na ‘airtime’ za kutosha katika redio na TV mbalimbali.

Foby naye anatarajiwa kuwa mmoja wa damu changa za kuchungwa kutoka na uwezo aliokuwa nao katika kupangilia mashairi hadi sauti ya kuimba.

sholo-mwamba-1

Sholo Mwamba

Katika Muziki wa Singeli ulikuwa wa aina yake mwaka jana kutokana na ushindani uliokuwepo kati ya Man Fongo na Sholo Mwamba.

Sholo ambaye alianza kusikika baada ya kushirikishwa Ngoma ya Kazi Kazi na Prof. Jay. Baada ya kazi hiyo aliibuka na ngoma yake ya Ghetto. Msanii huyu bado ni muhimili wa Muziki wa Singeli kwa sasa akiwa na Man Fongo hivyo ni damu changa za kuchungwa zaidi.

Zipo damu changa nyingi zinazotazamiwa kuburuza mwaka huu ambazo ni pamoja na Ibrah Nation, Hamadai, Man Fongo na wengine kibao.

Comments are closed.