The House of Favourite Newspapers

CHUNGA SANA, MITANDAO INAWEZA KUKUINGIZA CHAKA!

NI kona ya Boyfriend and Girlfriend kwa ajili ya vijana ambao bado wapowapo sana wakiha-ngaika huku na kule kutafuta mwenzi mwema wa kuingia naye kwenye ndoa.  

 

Katika uwanja huu, sera kubwa zaidi ni kuelezana ukweli hata kama unauma, lengo likiwa ni lilelile; kujenga uhusiano imara. Nilishasema huko nyuma, nakumbusha tena, maisha bora ya baadaye hutegemea na familia bora ambayo huanza na mume na mke. Mpo mpaka hapo marafiki zangu?

 

Yes! Tuendelee na madini yetu. Mada ya leo inatokana na maswali mengi ya aina moja niliyoyapata kwa muda mrefu kutoka kwa wasomaji mbalimbali. Ni wengi, lakini nitachapa maswali ya mfano ili uweze kujenga uelewa sawasawa wa mada hii ambayo naamini itakubadilisha.

 

KUTOKA KWA MSOMAJI:

“Pole na kazi kaka Shaluwa, kuna kaka nawasiliana naye. Kiukweli tumezoeana sana, juzi hapa amesema eti ananipenda na anataka kunioa. Mimi nipo Mbeya, yeye anaishi Dar es Salaam. “Hatujawahi kuonana, zaidi ya kuzungumza kwa njia ya simu tu. Nilifahamiana naye baada ya kukosea namba, ndipo tukakubaliana kuwa marafiki. Tafadhali naomba msaada wako maana ninachanganyikiwa kabisa. Ni kweli ananipenda? Naomba msaada wako.”

 

Mwingine huyu hapa: “Nimekutana na rafiki kwenye group moja la WhatsApp, tunawasiliana mara kwa mara, ninahisi kumpenda huyo msichana. Naye ana kila dalili za kunipenda, tatizo sijaanza tu kumweleza. Hivi, inawezekana kweli tukapendana kabla ya kuonana?” Bila shaka kuna picha umeipata kupitia maswali ya wasomaji hao wawili. Niliwaahidi kuandika mada gazetini ambapo ndipo wangepata majibu yao. Je, wewe upo kwenye kundi gani?

 

Umewahi kukutana na jambo hilo? Unadhani unaweza kumpenda mtu kabla ya kukutana naye? Sauti pekee inaweza kumfanya mtu ampende mwenzake kwa dhati na mapenzi yao yakadumu? Je, unaweza kuanzisha uhusiano na mtu usiyemjua na mapenzi yakadumu kiasi cha kufikia kuingia kwenye ndoa? Tutapata majibu kwenye mada hii. Twende darasani…

DARASA LINAANZIA HAPA

Je, inawezekana? Hili ni jambo la kwanza linalotakiwa kupatiwa majibu kabla ya kuendelea na mada hii. Huu ni mtazamo hasi. Jibu kwa kifupi tu ni haiwezekani. Utawezaje kumpenda mtu ambaye hujamuona? Lakini lazima tukubaliane kuwa, inawezekana kuanzisha uhusiano wa urafiki na mtu ambaye hujamuona na baadaye taratibu mtazoeana na kufahamiana, kisha mkikutana ndipo hisia zenu zinaweza kuthibitika iwapo ni za kweli au drama.

Marafiki misingi ya kumpenda mwingine ikoje? Kanuni zipo wazi; KUPENDA ndiyo jambo la kwanza, ambapo ukweli ni kwamba huanza na kutamani, sasa itawezekanaje kumtamani mtu ambaye hujawahi kukutana naye? Baada ya kupenda, kuna mambo mengine ya msingi ambayo ni muhimu kuzingatiwa ili kujihakikishia kwamba uliyempata ni mwenzi sahihi.

Kuna suala la kuchunguzana tabia n.k, yote haya yatawezekana vipi kufanyika kabla ya kukutana? Najua ni wengi wamekumbana na hili ninalolizungumzia hapa, unashindwa cha kufanya na kubaki gizani. Leo utarudi kwenye mwanga! Unajua chanzo cha yote hayo ni nini? Twende kwenye kipengele kinachofuata.

HUANZA HIVI…

Chanzo kikuu cha udanganyifu huu wa mapenzi huwa ni vyombo vya mawasiliano. Mfano mtu amepiga simu amekosea namba…mara anaanza ‘uko wapi? Haina neno, tunaweza kuwa marafiki?’

Mazoea yakizidi, kila mmoja huanza kumuuliza mwenzake vitu anavyopendelea na mambo mengine. Baadaye wanatongozana! Huelezana mambo mengi sana na ahadi nyingi wakiamini kwamba wanapendana kwa dhati! Linaweza kuwa darasa gumu kidogo, lakini lenye faida kubwa sana kwenu. Kwa madini zaidi, usikose wiki ijayo katika sehemu ya mwisho ya mada hii, USIKOSE!

Comments are closed.