The House of Favourite Newspapers

CHUNGA SANA, MITANDAO INAWEZA KUKUINGIZA CHAKA -2

HAPA kwenye Boyfriend and Girlfriend ndiyo sehemu pekee ambapo vijana ambao bado hawajaingia kwenye ndoa, hupata darasa zuri la mahusiano kwa lugha ya kwao. Ni sehemu ambayo ukweli ndiyo dira ya kona hii.

 

Naamini kuna mengi umeshayapata tangu kuanzishwa kwa safu hii. Nafurahi kupata maoni yenu kwa wingi, kwa hakika ndiyo hasa yananipa nguvu ya kutafiti zaidi matatizo yanayowa-sumbua vijana ambao wanahaha kutafuta wenzi sahihi wa maisha yao.

 

Ni wiki ya pili na ya mwisho tunaangalia namna ambavyo baadhi ya watu hujiingiza katika matamanio ya mapenzi baada ya tu ya kuwasiliana na patna mwingine bila kuonana, wakiwa na imani kuwa huenda wanapendana kwa dhati, kumbe ni kudanganyana tu.

 

Je, ni kweli unaweza kumpenda mtu kabla hujamuona? Je, mnaweza kuanzisha na kudumisha penzi la mbali kwa kupitia simu au mitandao ya kijamii? Hebu tumalizie mada yetu…

 

MAPENZI YA HISIA

Kimsingi sababu ya haya yote ni hisia tu. Njia ya mawasiliano inaweza kukoleza au kuimarisha uhusiano ambao tayari upo. Mfano kama unaishi Moshi na mpenzi wako yupo Mwanza, mnaweza kuboresha uhusiano wenu kwa kuwasiliana kwa njia ya simu, waraka pepe na mitandao ya kijamii.

 

Kinachotokea kwa marafiki wapya ambao wanahisi tayari ni wapenzi na wanapendana ni zile hisia za ndani zinazowaingia wakati wa mawasiliano yao. Pengine walianza kuzungumzia mambo ya mapenzi na kujikuta wakitamani kuwa karibu.

 

Jambo kubwa zaidi ni kwamba mhusika hutawaliwa zaidi na hisia, maana kwa sababu hawafahamiani, watakuwa wanauliza: ‘Wewe ukoje? Mrefu, mfupi, mwembamba, mnene au?’ halafu mwenzake atamjibu, ‘mrefu kiasi, si mnene sana, kifupi nina umbo namba nane…navutia na ni maji ya kunde’.

 

Mtu anaweza kujielezea vyovyote atakavyo, hivyo kumfanya mwenzake amtengeneze ajuavyo kichwani mwake na kujihakikishia kwamba anampenda kwa dhati mwenzake kumbe anajidanganya!

 

TABIA BANDIA

Mbaya zaidi ni kwamba, wakati wapenzi hawa wanaoji-danganya wakiendelea kuwasiliana si rahisi kujuana vizuri kitabia kwa sababu wengi huonesha tabia bandia. Mambo yao ya ndani wanayaficha kwa nguvu na kuonesha mema tu. Hapo ndipo mwanzo wa penzi feki kwa kudanganyika na tabia za kutengeneza.

 

HULKA MBAYA

Kuna wengine ni tabia zao za asili. Amezoea kupata wapenzi kwa kupitia kwenye simu na mitandao ya kijamii. Usishangae kuna wengine wanapiga namba hata wasizozijua, akikutana na mtu wa jinsia tofauti na yake, anaanza mambo yake. Akimaliza haja zake anakuacha!

 

ACHA KUJIDANGANYA

Ni vizuri sasa ukatoka kwenye ulimwengu wa giza na kurudi kwenye ulimwengu unaoonekana. Kwa hakika ni vigumu sana kumpenda mtu ambaye hujamuona, labda kama unataka kucheza na muda wako. Wako anakuja, vuta subira ukifanya mambo yako kwa usahihi. Usijida-nganye na matapeli wa mapenzi. Wapo baadhi ambao wanafanikiwa kuingia kwenye mapenzi lakini mwisho wao hauwi wenye mafanikio.

 

Penzi la dhati hubebwa na vitu vingi sana, ukiachana na UPENDO kuna suala la tabia na mengine mengi ambayo huwezi kuyajua kwa njia ya kuwasiliana pekee. Utajihakikisha umempenda kwa kumtengeneza kichwani mwako, mwisho wa siku unakutana na mtu ambaye yupo tofauti na mawazo yako, itakuwaje hapo?

 

Nasisitiza, ni sahihi kuanzisha urafiki, lakini kamwe msiingie kwenye mapenzi kabla ya kuonana, maana zipo gharama zake! Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa vinavyopatikana kwa oda.

Na Joseph Shaluwa, Simu 0718 400146

Comments are closed.