Chuo Cha UDSM Chapatiwa Dola Milioni 47.5 Kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimepatiwa Dola za kimarekani milioni 47.5 sawa na zaidi ya bilioni 100 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)
Akizungumza mwanzoni mwa wiki Zanzibar Mratibu Msaidizi wa Mradi wa HEET kutoka UDSM Dkt. Liberato Haule amesema kuwa Kupitia fedha hizo sehemu kubwa inatumika katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, kuandaa na kuboresha mitaala ili iweze kuendana na soko la ajira ambapo mitaala takribani 98 ipo hatua za mwisho za kuweza kupata Ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
“Kazi nyingine zinazotekelezwa ni pamoja na kuanzisha kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera na kujenga na kuboresha miundombinu katika kampasi kuu ya Dar es Salaam na Buyu-Zanzibar” amesema Dkt. Haule
Dkt. Haule ameongeza kuwa shughuli zote zitakapokamilika zitaongeza madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wapatao 2,120, karakana zenye vifaa zitakazokuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 90, maabara ambazo zitafungwa vifaa zenye uwezo wa kutumiwa na wanaafunzi 830 na mabweni ambayo yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 452
Aidha, katika kuhakikisha chuo hicho kinatoa wahitimu wanaendana na soko la ajira kupitia Mradi wa HEET kimeanzisha kamati za makampuni na waajiri (industrial linkage committee) ambao wanashiriki katika zoezi zima la uandaaji wa mitaala na ufundishaji kwa sababu wao ndio watumiaji wa wanafunzi hao na imefanikisha kutengeneza miongozo mbalimbali ya namna ya kuwashirikisha katika uandaaji wa mitaala na wanafunzi
Mratibu huyo ameongeza kuwa Mradi umefadhili walimu wapatao 23 kwenda masomoni katika vyuo vikuu vikubwa Duniani katika ngazi za uzamivu na uzanivu ambapo mpaka sasa kati ya hao walimu nane wameshahitimu masomo
Kaimu Mkurugenzi wa moja ya Taasisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Buyu Zanzibar ya Sayansi za Bahari Dkt. Saidi Sagamaneno amesema taasisi hiyo imenufaika na Mradi wa HEET ambayo imepata bilioni 11 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na taaluma, hosteli za wanafunzi na ukumbi wa mikutano utakaokuwa na uwezo wa kuchukua watu 150
Dkt. Sagamaneno amesema
Ujenzi huo utakapokamilika utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 139 hadi kufikia 278.
Naye Mkuu wa Taasisi ya UDSM inayoshughulika na masuala ya Jinsia Dkt. Lulu Mahai amesema Taasisi hiyo imenufaika kwa kujengewa Kituo kitakachosghulikia masuala ya jinsia na elimu maalum pamoja na kununuliwa vifaa vya kuwasaidia wanafunzi na watumishi wenye mahitaji maalumu.