The House of Favourite Newspapers

Chuo Kikuu Cha UDSM Kuadhimisha Wiki Ya Utafiti na Ubunifu

0
s

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeutaarifu umma wa watanzania na kuwaalika wadau wa elimu na maendeleo, kwa ujumla kushiriki katika Maadhimisho ya Nane ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yatakayoanza saa 2:00 asubuhi siku ya tarehe 23 Mei 2023 katika eneo la Maktaba ya Chuo iliyoko Mlimani na kufunguliwa na Mgeni Rasmi ambaye ni Mhe. Profesa Adolf Faustine Mkenda (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti, Prof. Nelson Boniface amesema kuwa Maonesho hayo yaatarajiwa kuhitimishwa siku ya tarehe 25 Mei 2023 saa 10:00 jioni ambapo  tukio hilo muhimu litahusisha hotuba kuu, mazungumzo ya mashirikiano ya kimkakati, kongamano, maonesho na mawasilisho ya watafiti na wabunifu likiwa ni jukwaa la washiriki kupata fursa ya kubadilishana maarifa na ushirikiano.

Ni kwa msingi huo, siku ya ufunguzi kutakuwa na Wazungumzaji wakuu (Keynote Speakers) wawili ambao ni mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Ndege ya Precision Air ndugu Michael Shirima na mwingine ni Profesa Leticia Rutashobya, kutoka Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Utafiti na ubunifu ni vichocheo muhimu vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivo basi kutokana na malengo ya kuanzishwa kwake UDSM inawajibika kuandaa na kusaidia watafiti na wabunifu wenye uwezo wa kutambua changamoto zinazoikabili Tanzania na kutafuta ufumbuzi. Kaulimbiu ya Maadhimisho haya ya nane ni Manufaa ya Utafiti na Ubunifu kwa Ustawi wa Uchumi-Jamii Tanzania.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatumia fursa hiyo kujipambanua kwa jamii kwa kuonesha shughuli zake za utafiti, ubunifu, huduma kwa umma na ubadilishanaji maarifa kwa kuzingatia MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2021/22 – 2025/26 wenye wito wa Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Wiki hii pia hutoa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wadau mbalimbali kitaifa na kimataifa hivyo, siku ya pili, Jumatano 24 Mei 2023, asubuhi kutakuwa na mazungumzo maalum ya mashirikiano ya kimkakati yatakayo washirikisha wadau kutoka katika sekta binafsi, za umma na vyombo vya habari. Baadaye mchana wa siku hiyo hiyo kutakuwa na

kongamano litakalowahusisha wabobezi katika masuala utafiti na ubunifu kwenye maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano; maendeleo ya sayansi akua na bahari; maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi; historia, utamaduni na turathi; na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kutoka taasisi mbalimbali.
Maadhimisho haya pia yatatumika kutambua michango iliyotukuka ya wanataaluma na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti, ubunifu na ubadilishanaji wa maarifa. Hivyo, katika sherehe za kufunga Wiki ya Maadhimisho haya tarehe 25 Mei 2023, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo atatoa tuzo kwa watafiti na wabunifu waliofanya vizuri zaidi katika makundi yafuatayo:
1. Mradi Bora wa utafiti,
2. Vitengo/Idara Zilizoingiza Kiasi Kikubwa cha Fedha za Utafiti,
3. Vitengo/Idara Zilizoingiza Kiasi Kikubwa cha Fedha za Ubunifu,
4. Watafiti Walioingiza Kiasi Kikubwa cha Fedha za Utafiti,
5. Utambuzi wa Mtafiti Hodari wa Mwaka,
6. Utambuzi wa Mbunifu Hodari wa Mwaka,
7. Miradi Bora wa Wanafunzi wa Uzamili,
8. Miradi Bora wa Wanafunzi wa Shahada za Awali, na
9. Miradi bora wa Huduma kwa Umma.
Hivyo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawaalika wadau wote wa Elimu Nchini, Jumuiya ya Wahitimu, Viongozi wa Serikali, Wadau wa Maendeleo, Mabalozi, Viongozi wa Kisiasa, Viongozi wa Vyama vya Kiraia, Waandishi wa Habari na Wananchi Wote kwa ujumla kushiriki katika Wiki ya Utafiti na Ubunifu ili tuweze kujifunza na kubadilishana mawazo kwa Ustawi wa taifa letu.

 

Leave A Reply