The House of Favourite Newspapers

CHUO KIKUU HURIA CHAREJESHA PROGRAMU YA MAANDALIZI

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Bisanda akizungumza na waandishi wa habari leo (hawapo pichani).

 

 

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) kimeutaarifu umma kuwa programu ya maandalizi (foundation programme) imerejeshwa rasmi baada ya kufanyiwa maboresho kama ilivyoelekezwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TVV)

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Elifas Tozo Bisanda amesema kuwa lengo kuu la programu hiyo ni kuwaongezea uwezo wanafunzi waliopungukiwa kwa kiasi kidogo, sifa za kujiunga katika vyuo vikuu nchini kwa vigezo vilivyowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TVV).

 

Alisema wanafunzi wanaodahiliwa katika programu hiyo wanapata fursa ya kuelewa mbinu mpya za kujifunza kwa njia ya masafa hususani matumizi ya TEHAMA katika kujifunza  na hivyo kwa wale watakaobahatika kujiunga na masomo ya shahada kwa njia ya masafa kupitia chuo hicho watakuwa wameandaliwa vyema kufuata mfumo huo ambao ni wa kisasa zaidi katika kupata elimu ya juu.

 

“Ni kweli kwamba kulikuwa na programu nyingine ambazo hazikuwa na ubora wa kutosha kuwaandaa wanafunzi kuingia katika masomo ya shahada,” alisema.

 

Aidha ameeleza kuwa kutokana na maboresho yaliyotakiwa kutoka TVV chuo hicho kilifanya maboresho ambayo yalitakiwa na kupatiwa ithibati ya programu hiyo mpya.   Hivyo kufuatia maboresho hayo,  wahitimu wa programu hiyo watakaofaulu kwa vigezo vilivyowekwa wataruhusiwa kujiunga na shahada ya kwanza katika chuo kikuu chochote nchini.

 

Programu hii ya mwaka mmoja inalenga kuwadahili wenye sifa zifuatazo:

A. Wahitimu wa kidato cha sita wenye ufaulu wa angalau pointi 1.5 katika masomo mawili;

B. Wahitimu wa stashahada kutoka vyuo vinavyotambuliwa na serikali wenye ufaulu wa GPA ya kuanzia 2.0; na

C.  Wahitimu wa ‘NTA Level 5/Professional Technician Level II Certificate’.

 

Kwa maelezo hayo, wahitimu wa kidato cha nne na wenye cheti (astashahada) ambao hapo awali waliweza kudahiliwa katika kozi hii, sasa wanashauriwa kujiunga na kozi za stashahada na iwapo watafaulu vizuri stashahada na kupata sifa zinazokubaliwa, wataweza kuendelea na masomo ya shahada.

 

Maombi ya kujiunga na programu yalianza kupokelewa tangu Aprili 10 mwaka huu na udahili utaendelea hadi Agosti 31.  Waombaji pia wametakiwa kutembelea tovuti ya chuo (www.out.ac.tz),

 

Mnamo Julai 2016, TVV  ilitangaza kusitishwa kwa programu zote za maandalizi (Foundation Programme) zilizokuwa zinatolewa na vyuo mbalimbali.

 

 

Comments are closed.