The House of Favourite Newspapers

Chuzi Akwaa Balaa Jingine!

0
Mr. Chuzi.

IKIWA bado lile sakata lake na Chama cha Waigizaji kupelekana mahakamani halijapoa, msanii nguli wa tamthiliya Bongo, Tuesday Kihangala ‘Mr. Chuzi’ amezua balaa jipya ambapo awamu hii baadhi ya wadau wa sanaa wameibuka na kumsakama kwa ukimya wake kwani wanakosa ladha na burudani stahiki waliyoizoea kutoka kwake.

Katika mazungumzo na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, wadau hao walionesha kukerwa na kitendo cha Chuzi kukatisha Tamthiliya ya Closed Chapter iliyokuwa ikiruka kupitia Runinga ya Taifa, TBC1 na kwamba wanamtaka arejeshe makali yake kama ilivyokuwa kwenye Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu iliyokuwa imesheheni visa na mikasa ya kusisimua.

“Kwa kweli Chuzi hatumuelewi, ameondoa Tamthiliya ya Closed Chapter iliyokuwa ikiruka TBC1 tena bila maelezo na sasa hivi kakuna kinachoendelea, aturudishie ladha yetu kwenye tamthiliya, tunakosa burudani,” alisema Nasma aliyejitambulisha kama mdau wa sinema na filamu Bongo.

Kwa upande wake, Chuzi alipotafutwa na mwandishi wetu na kusomewa madai hayo, alisema alisitisha tamthiliya ya Closed Chapter TBC1 kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake na kwamba hadi sasa yuko Lushoto akiandaa mzigo mwingine ambao utaruka hivi karibuni.

“Kuna sababu za msingi ambazo zilinifanya nisitishe tamthiliya ya Closed Chapter lakini hadi sasa niko Lushoto nikiandaa kazi nyingine ambayo ni kali na nzuri zaidi na kwamba natarajia wadau wataipenda na kuipokea kwa mikono miwili kabisa na mimi nipo na nitaendelea kuwapa burudani na elimu kupitia sanaa,” alisema Chuzi.

BRIGHTON MASALU

Leave A Reply