Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-14

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Musa vipi? We unajua namba yako sina, kwa nini usinitafute wakati we unayo? Kwani ule ujumbe wangu asubuhi kupitia kwa mtoto hukuuelewa?”
JIACHIE MWENYEWE SASA…

“Ujumbe upi?” aliuliza Musa…
“We si tulipanga tukitoka job unipigie!”
“Tuliongea wapi mama Shua?”

“Kwani hukunielewa muda ule asubuhi ulipokuwa unajibizana na mwanangu Shua?”
“Oh! Kumbe pale ulikuwa unanipa ujumbe wa moja kwa moja siyo?”
“Sasa je?”
“Ungesema sasa.”

“Sasa pale ningesemaje we unavyodhani?”
“Basi yaishe…sevu upya namba zangu.”
“Zitaje, lakini sitazisevu, nitaziweka kichwani tu.”
“Sawa,” alijibu Musa huku akimtajia mama Shua namba zake.

Kisha, haraka sana mama Shua alirudi ndani akimtaka Musa kuchelewa hata dakika tano ndipo aingie…
“Usiingie sasa hivi, itajulikana. We kaa kwanza mahali, baada ya dakika tano ingia, sawa mpenzi wangu?”

“Sawa. Lakini da! Jamaa naye anafuatilia sana bwana,” alisema Musa akirudi alikotoka.
Alikwenda kwenye duka la jirani na kuomba soda ili apotezee muda. Alikunywa, alipomaliza alikwenda kwake. Ni baada ya dakika kama kumi na mbili hivi.
Chumba kilikuwa kizito kwa Musa kwani muda mwingi alijikuta akimuwaza mama Shua na mambo yaliyojitokeza kuhusu mume wake…

“Nahisi hii nyumba si ya kuishi mimi. Kama ndani ya mwezi mmoja tu jamaa ameshtuka kitu. Je, nikikaa mwaka mmoja si nitakatwa masikio mimi!”
***
Kwa upande wake, mama Shua hali ilikuwa ya utulivu wa kimawazo. Yeye alishatekwa na kijana huyo hivyo alikuwa akiwaza namna atakavyodumisha penzi…
“Musa ni kijana mzuri sana. Lakini sasa itakuaje wakati mista naye kama hataki kumsikia achilia mbali kumwona?” alijiuliza, akakosa jawabu.

Muda ulivyozidi kwenda, alipanda kitandani akalala. Alitamani sana kumtumia meseji Musa lakini mume wake alishalala hivyo aliamini angeweza kuzua mapya jambo ambalo hakulipenda hata kidogo!
***
Kulikucha, oyaoya za kujiandaa ndani ya nyumba zilipamba moto. Baba Shua, mama Shua, Shua walikuwa uani na msichana wa kazi. Musa yeye alivaa bukta na singilendi huku taulo akilitupia begani kwa ajili ya kwenda kuoga.

“Hujambo mchumba?” alianza Musa. Safari hii alikuwa tayari kupokea ujumbe kutoka kwa mama Shua kama alivyomwambia jana yake…
“Mwambie sijambo, nimekumisi sana.”
“Jambo…misi sana.”

“Hata mimi. Sasa leo tutapata wapi lanchi mchana mchumba?”
“Mwambie unipigie, popote ulipo nitakuja.”
“Nakuja…”

Walicheka wote kwani Shua alishindwa kunyoosha Kiswahili, Musa akaendelea…
“Mchumba, kweli utaweza kuja nikikuita mahali kwa ajili ya lanchi?”
“Mwambie nitaweza bila shida,” hapo alisema baba Shua…
“Aweza.”

“Haya, basi nitakupigia.”
“Mwambie sawa usikose, iwe saa saba kamili,” hapo alidakia mama Shua…
“Saa saba …amili.”

Walicheka tena, Musa akaingia kuoga chapuchapu. Alitoka, akaingia mama Shua. Yeye alioga akifurahia kusikia raha anaoga huku akiyaona majimaji yaliyobaki kwa kuoga Musa.
Alipomaliza naye alitoka kwa kasi akisema amechelewa sana siku hiyo…
“Mbona siku ile nakwenda Arusha ulichelewa sana na sikukusikia ukilalamika. Imekuaje leo?” aliuliza baba Shua.

“Hata siku ile nililalamika, sema sikukwambia tu.”
“Mh!” Aliguna baba Shua.
Musa alitoka, wakati anapita kwenye dirisha, mama Shua alimwona, naye akajiandaa haraka sana huku moyoni akisema…

“Kwani akinipa lifti mbele kwa mbele kuna tatizo gani? Yaani mume wangu yeye anawaza mabaya kila wakati.”

Tangu, Musa atoke, mama Shua alitumia ndani kama dakika tano, naye akatoka lakini alishamtumia meseji Musa kumwambia amsubiri ampe lifti. Na Musa naye alijibu…
“Mh! Huogopi?”
“Wala!” alijibu mama Shua.

Mama Shua alitoka mbio kiasi kwamba mumewe akashtuka sana…
“Kinachokufanya ukimbie ni nini mama Shua?”

“Nawahi baba Shua, si nimekwambia wakati natoka kuoga jamani mume wangu!?” alijibu mama Shua huku akikimbia kitendo kilichomfanya baba Shua kushindwa kuendelea kuhoji au kusema lolote jingine.
Mama Shua alipotea akimuwahi Musa, mumewe akiwa ndani ya bukta na singilendi kwa juu naye alitoka mbio akimwambia msichana wa kazi…
“Dada nakuja sasa hivi.”

Mbele kidogo, baba Shua alikutana na Bajaj inashusha abiria…
“Eee bwana niwaishe mahali,” alimwambia suka wa Bajaj.
Bajaj iligeuzwa kwa kasi kutokana na hali ya uso wa baba Shua, dereva akajua anawahi sehemu kwa dharura.
“Nipeleke kule, kanyaga mafuta kama unafukuza mwizi.”
***
Mama Shua alizama ndani ya gari la Musa…
“Ondoa gari, maana kama sijamuelewa mume wangu, anaweza akafuatilia,” alisema mama Shua.

Ile anafunga mlango tu, Bajaj aliyopanda mume wake ikatokea kwa mbali kidogo.
Baba Shua alitumbua macho mbele akiamini kama mke wake atakuwa anaondoka na daladala lazima angemwona anakaribia kituoni na kama hayupo, ina maana atakuwa ndani ya gari analoliona la Musa ambalo yeye baba Shua halijui.
Je, nini kitaendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa, siku ya Ijumaa.


Loading...

Toa comment