The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-19

0

Turkey-Drumstick-Stew_36_1.1.300_326X580ILIPOISHIA IJUMAA ‘KUBWA’:
Mama Shua alibaki ameduwaaa asijue la kufanya kwani majibu ya mama yake yalimpa picha kamili ambayo hakuwahi kuiona hata siku moja.
JIACHIE MWENYEWE SASA…

“Loo! Yamenikuta…huyo mzee wa nyumbani aliyeniona hotelini mpaka akapeleka umbeya huu kwa mama sijui nani?” alijiuliza moyoni…

“Lakini kwani lazima nikiwa naingia hotelini iwe kwa sababu ya kufanya zinaa? Kwa nini mama asiniulize mimi kwanza halafu jibu langu ndiyo likatoa mwanga wa uamuzi wake?” aliendelea kujiuliza mama Shua, alikosa raha. Pia akakosa amani ya moyo.
Palepale akampigia simu mdogo wake, Selina…
“Ee dada…”

“Selina, ni kwa nini mama anatoa maamuzi bila kuniuliza mimi akasikia nitajibuje?” aliuliza palepale mama Shua…
“Kivipi?”

“Yeye ananihukumu tu kwa vile kasikia eti nimeonekana nikiingia na kutoka baa…anajua nilifuata nini? Pengine niliingia kuzungumza na mtu je? Hotelini si kunakuaga na ukumbi wa mikutano!”

“Dada Sesilia….mama akuulize wakati yule mzee amekuwa akikuona ukiingia chumbani na unakaa sana humo! Huo ukumbi upo chumbani dada Sesilia? Unajua mpaka ile presha ya mama ilishuka! Yaani wewe dada Sesilia…mh! Mi mwenyewe sijaamini hata kidogo…yule mzee akasema alikusalimia kwenye korido ukampotezea.”

Mama Shua alikata simu. Hakuwa tayari kuendelea kusikia maneno yenye maumivu makali kama hayo…

“Mh! Yule mzee akasema alikusalimia kwenye korido ukampotezea’,” mama Shua aliyarejea maelezo ya mdogo wake kiasi kwamba, alitamani ardhi ipasuke.
Alipowaza sana, mama Shua akakumbuka kwamba, ni kweli siku moja akiwa anatoka kwenye hoteli anayokutanaga na Musa, alimwona mzee mmoja ambaye aliachia tabasamu na akamsalimia.

Alikumbuka kwamba, sura ya mzee huyo haikuwa ngeni machoni pake lakini aliamini ni wazee wa Jiji la Dar es Salaam ambao wanapenda dogodogo!
“Aaaa! Mzee Magunia…yule aliyenisalimia siku ile ni mzee Magunia wa kijijini kwetu…da! Ndiyo maana nilijiuliza huyu mzee mbona kama namfahamu vile! Lo!”
***
Mchana wa saa saba, Musa alimtumia meseji mama Shua…
“Haloo…”

Mama Shua baada ya kuisoma meseji hiyo alisonya, akasema moyoni…
“Ungejua ulivyoniletea matatizo wala usingetuma helo zako.”
Musa alipoona hajibiwi na mama Shua aliamua kupigia simu. Iliita weeee! Mpaka ikakatika! Ikaita tena wee mpaka ikakatika…

“Khaa! Huyu ana nini sasa?” alijiuliza Musa. Akapiga tena…simu ikaita weee mpaka ikakatika! Akamtumia meseji…
“Kuna tatizo baby?”

Meseji hiyo haikujibiwa, Musa akasema moyoni kwamba kama angekuwa anapajua ofisini kwa mwanamke huyo angekwenda ili akajue kuna nini kilichotokea!
Baada ya nusu saa, baba Shua alimtumia meseji mkewe…
“Kama mama amejua uovu wako, ni zaidi sana mimi. Jua umesimama katikati. Unaweza kuingia au kutoka. Lakini yote hayo yametegemea maono ya moyo wako katika kuamua baya na zuri.”

Mama Shua alijikuta akichukia sana, akamjibu…
“Unahukumu kama mchungaji au hakimu?”
“Kama wote…”

“Ungechunguza kwanza kabla ya kusema…”
“Namshukuru Mungu nimechunguziwa na mama yako.”
“Niache tafadhali…nataka niendelee na maisha yangu…”
“Uachwe mara ngapi?”

“Basi hakuna haja ya meseji zako,” alisema mama Shua. Lakini naye akawa hajui mumewe amemwacha kwa maana gani? Kwamba hamtumii tena meseji…hamfuatifuati na mambo yake au anamwacha kwa maana ndoa basi tena!
Kweli, baba Shua hakutuma tena meseji kwa mama Shua kiasi kwamba, mwanamke huyo alichanganyikiwa.
***
Muda wa kutoka kazini ulifika, mama Shua alitamani siku hiyo asirudi nyumbani kwake kwa mambo yaliyotokea. Alijisikia kulalalala mahali mpaka saa mbili usiku au tatu ndipo arudi nyumbani. Lakini kama angekwenda kulala mahali, angekuwa na nani? Maana kuwa peke yake pia ilikuwa tatizo, mawazo yangekuwa palepale. Alihitaji kampani, tena ya mwanaume. Ilibidi amkumbuke Musa.
Aliaga wenzake akatoka, nje akampigia simu Musa…

“Uko wapi baby?”
“Niko baa…we si unasikia kelele hapa!”
“Baa wapi?”
“Posta.”
“Tunaweza kuonana?”
“Wapi?”

”Wapi! Si kule mahali kwetu!”
“Saa ngapi?”
“Mimi ndiyo nimetoka, naelekea.”
“Oke, nakuja.”

“Please, usichelewe baby.”
Mama Shua alichukua usafiri, ukampeleka hadi kwenye hoteli hiyo. Alishuka, akamalizana na mwenye usafiri, akatembea mpaka mapokezi. Alilipia chumba yeye mwenyewe, akapelekwa chumbani.

Alikuwa ameshavua nguo, amejifunga taulo tu na alilala kitandani simu ikiwa mkononi akianza kuchati. Kwanza kabisa alimtumia meseji mumewe…
“Natoka kazini napitia kwa rafiki yangu Rukia… kuna ishu ya kuzungumza naye…”
Hakujibiwa meseji hiyo lakini yeye hakujali, akamgeukia Musa…
“Mimi nimeshafika, wewe uko wapi baby?”
“Nakaribia baby,” alijibu Musa.

Mara, ikaingia meseji nyingine. Hii ilitoka kwa mama yake kijijini…
“Kwa hiyo hiyo hoteli ndiyo umeigeuza nyumbani kwako sasa??!!”

Leave A Reply