Chuzi ndo hilo, hakuna kuonja!-22
ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Sasa unadhani itakuwaje na mtu kasimama mlangoni!”
Pale nje, baba Shua aliwaza kuwagongea mlango wawili hao ili ijulikane moja.
JIACHIE SASA…
Aliwaza sana, akaamua kwamba amwambie msichana wake wa kazi ni marufuku kufungua mlango wa chumba cha Musa endapo ataambiwa afanye hivyo…
“Ngo ngo ngo,” aligonga.
Msichana wa kazi akafungua na kusimama mlangoni…
“Dada, mama Shua ameingia kwenye chumba cha yule kijana mgeni…”
“Haa! Kufanya nini?”
“Anajua mwenyewe…sasa sikia, akikupigia simu ukamfungulie mlango usiende maana ni mimi nimefunga kwa nje…”
“Ha! Sasa dada kaenda ndani kwa watu kufanya nini tena jamani? Halafu mbona ni usiku sana?”
“Mama Shua si mwaminifu,” alisema baba Shua huku akiondoka kurudi chumbani kwake.
Alipanda kitandani kulala, akaanza kuwaza kabla ya kuupata usingizi…
“Siwezi kuwa na ndoa tena…na nikisema nimvumilie nitakuwa mwanaume wa ajabu wa kwanza hapa duniani,” alisema moyoni baba Shua. Usingizi ukampitia haraka.
***
Kule chumbani, mama Shua na Musa walikaa tu juu ya kitanda. Muda mwingi mama Shua alikuwa akimwaga machozi. Kuna wakati alimwingiza akilini mama yake mzazi, akajikuta akiogopa zaidi…
“Musa, unadhani itakuwaje sasa?”
“Kuhusu nini?”
“Mimi naachwa mwenzako. Kwani we hujui?”
“Da! Sasa tufanyeje mama Shua?”
“Mi sijui.”
Hakuna aliyelala, muda mwingi walikuwa wakisinzia lakini bila kulala. Mama Shua hakumpigia tena simu msichana wake wa kazi baada ya kujua kuwa, mumewe amesimama mlangoni…
“Yaani najuta mimi najuta! Nilikuwa nakosa nini kwa mume wangu mpaka kujikuta natumbukia kwenye penzi la nje. Nitamwambia nini mama?” alisikitika mama Shua huku machozi yakiufunika uso wake.
Jogoo la kwanza liliwika, mama Shua akashtuka sana…
“Umesikia jogoo hilo?” alimwambia Musa…
“Kumekucha,” alisema Musa huku akiuendea mlango na kujaribu tena kuufungua, akakuta umefungwa vilevile. Akarudi kitandani huku akisikitika sana…
“Da! Mlango bado umefungwa mama Shua…mumeo sijui amenikusudia nini mimi! Mwenyewe najuta sana na hii hali…unadhani nitaendelea kuwa mpangaji kwenye nyumba hii?”
“Uendelee, usiendelee mimi sijui Musa. Kwani sitakuwepo tena.”
Kulikucha kabisa, mlango bado ulifungwa kwa nje. Msichana wa kazi wa mama Shua alishaamka na kuendelea na kazi zake za kila siku huku akijua mama Shua yumo chumbani kwa Musa. Alijiuliza mengi moyoni.
Jua lilichomoza, mama Shua akapata wazo kwamba achukue simu ya Musa, ampigie baba Shua na kumwomba afungue mlango atoke, achukue mizigo yake na kuondoka kabisa lakini Musa akagoma kumpa simu yake…
“Noo mama Shua…siwezi kukupa simu yangu wakati najua yule ni adui yangu…siwezi. Kama anataka tufie humu ndani poa tu. Kama amepanga kuniua mimi sasa nitafanyaje?” alisema Musa akiwa amekasirika sana. Kwake, ilifika mahali ikawa liwalo na liwe.
Jua lilitoka kabisa, baba Shua alitoka chumbani na Shua, akaenda kuufungua mlango na kumwingiza Shua ndani…
“Nenda kwa mama yako.”
Mama Shua alishtuka sana kumwona mtoto wake akiingia na mlango ukiwa umefunguliwa. Alimkumbatia na kuanza kulia huku akisema…
“Mwanangu, nimekutenda vibaya sana. Utahangaika sana kwa sababu ya akili mbaya ya mimi mama yako.”
Shua hakujua lolote. Alibaki akimwangalia mama yake kwa macho ya mshangao…
“Mamaa,” aliita Shua, mama Shua akazidisha kilio kumsikia mtoto wake akimwita mama.
Shua aliachana na mama yake, akamfuata Musa…
“Chumba…”
Musa alikasirika sana, akatamani kumpiga. Shua alimwita Musa chumba kutokana na maneno yake siku za nyuma akimtania Shua kwa kumwita mchumba.
***
Baba Shua alikwenda kuoga, akavaa na kuondoka zake huku pesa za matumizi akiwa amemwachia msichana wa kazi.
***
Muda f’lani, mama Shua alisimama mlangoni akimlia taiming msichana wake wa kazi akipita…
“Dada,” alimwita alipopita…
“Abe…shikamoo dada…eti kwa nini upo huko?”
“Hayakuhusu…baba Shua ameondoka au yupo?”
“Ameondoka.”
“Kweli?”
“Kweli ameniaga, ameniachia pesa za matumizi.”
Mama Shua alirudi chumbani, akamchukua Shua na kutoka akiwa hana hamu tena na Musa.
Aliingia chumbani kwake. Kitu cha kwanza ni kuangalia simu yake, akaikuta. Akashangaa sana kwani aliamini jambo ambalo angelifanya baba Shua ni kuondoka na simu hiyo.
Aliipekua ndani na kubaini kwamba, haijachunguzwa kwani baadhi ya meseji zilikuwa za jana yake usiku na hazikusomwa.
“Mh! Sasa hapa dawa ni kumwomba radhi baba Shua. Mimi ni mkewe wa ndoa, binadamu hukosea, hiyo ni kawaida. Naamini atanisamehe tu. Nitamwambia sirudii tena, nimwahidi uaminifu,” alisema moyoni mama Shua.
Amwombeje samahani? Aliamua kumwandikia ujumbe wa simu badala ya kumpigia akiamini kwa kusoma atamwelewa vizuri zaidi kuliko kumwendea hewani. Kwanza anaweza asipokee hata hiyo simu yake. Aliandika:
“Baba Shua, najua kosa langu, nimekutenda vibaya sana mume wangu. Nakiri kosa moja kwa moja. Niko chini ya miguu yako mume wangu, nisamehe sanasana! Sitarudia tena, ni shetani tu alinipitia. Sasa nimejitambua ujinga wangu. Please mume wangu. Nisamehe saba mara sabini.” Akatuma.