The House of Favourite Newspapers

Chuzi Ndo Hilo, Hakuna Kuonja!-32

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
Jome yeye hakusalimia yeyote yule, naye akafuata nyuma ya Maua. Baba Shua akafuatia, wakaingia kwenye gari na kuondoka.
***
“Musa,” aliita mama Shua…
“Vipi?”
SASA SHUKA NAYO SASA…

“Ee! Chuzi ndiyo hilo sasa…hakuna kuonja.”
“Una maana gani mama Shua?”
“Nimeshaachika, hakuna tena ndoa.

Sasa wewe uliyeniharibia usije ukaniacha. Ulikuwa unanitaka kwa machale ukimwogopa mwenye mali, sasa kaniacha ndiyo maana nasema chuzi ndiyo hilo hakuna kuonja,” alisema mama Shua kwa sauti ya uchungu huku machozi yakimchuruzika…
“Mama Shua, kwanza nataka kukwambia siko tayari kuonekana mimi ndiye chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yako.”

“Heee! Musa una akili kweli wewe? Yaani wewe ndiye chanzo halafu mara hii unataka kujitoa? Kwa taarifa yako sasa, mimi sijawahi kuchepuka tangu nimefunga ndoa. Ndiyo kwanza kwako…”

“Kwani mimi na wewe mama Shua nani alianza kumtongoza mwenzake?” aliuliza Musa kwa sauti ya juu sana…
“Wewe…”

“Una kumbukumbu vizuri? Wewe hukumtuma msichana wako wa kazi aombe namba yangu ya simu? Wewe si ndiye ulikuwa unanitumia meseji zako za kuniuliza kama nimeshakula? Kwani kuna siku nilikwambia huwa nashinda njaa? We vipi bwana!” Sasa Musa alikuja juu kiasi kwamba, baadhi ya wateja walianza kuhisi kitu kutoka kwenye meza yao.
***
Baba Shua alifika nyumbani, akachukua nguo, viatu, sendozi, mikanda, soksi na makufuli, akatumbukiza kwenye begi moja kubwa na kuondoka. Maua alimsubiri kwenye gari kwa mbali kidogo. Hapo walikuwa wameshatengana na Jome ambaye alishuka mahali na kuendelea na mambo yake.

Waliondoka, baba Shua ndiye aliyekuwa akiendesha mpaka Kimara nyumbani kwa Maua. Maua alifurahi kupita kiasi. Aliamini sasa Benny amekuwa wake tena kwani kati ya mambo yaliyokuwa yakimnyima raha ni kitendo cha umri kukatika na hakuna mchumba anayejitokeza…

“Benny,” Maua aliita wakiwa wanakula…
“Yes!”
“Mpango wako ni nini juu na mkeo na mimi?”

“Maua, acha kumtaja yule mwanamke kwenye akili yangu. Sitaki presha, sitaki aina yoyote ya mawazo juu yake. Mimi niko kwako Maua…Kama na wewe utakuja kunifanyia tukio kama lile, basi mtakuwa mmeamua kuniua,” alisema kwa hasira baba Shua huku akiwa amemtumbulia macho demu wake huyo.
***
Kule hotelini, Musa alifika mahali akaondoka kwa hasira na kumwacha mama Shua ambaye alibaki akimwaga machozi tu. Ndoa chali, mpenzi naye chali! Alilia sana akijutia uovu wake.

Alijikongoja, akaenda kupanda bodaboda mpaka nyumbani kwake ambapo alimkuta msichana wake wa kazi na mtoto wake, Shua wakiwa nje…
“Vipi, mbona nje?” aliuliza mama Shua akiwa na hali ya mshangao…
“Baba,” alisema Shua huku akinyoosha mkono.

“Baba kafanyaje? Eti dada Shua anamaanisha nini?”
“Baba kaja, akachukua begi kubwa, sijui ni nini, akaondoka akisema kwa heri ya kuonana. Sasa Shua alikuwa anamlilia.”

Mama Shua alianguka chini na kupoteza fahamu. Alipokuja kuzinduka, alishangaa kujikuta katikati ya majirani akiwa amelala kwenye kochi kubwa sebuleni…
“Pole mama Shua…”

“Pole jirani yangu…”
“Jamani mama Shua pole…kwani ni nini?” majirani walimpa pole nyingi.
Alipepesa macho, akamwona mwanaye, Shua, akaanza kulia…
“Jamani kwani nini mama Shua?” majirani walimuuliza…
“Baba yake huyu ameondoka.”

“Kwenda wapi?”
“Eti amenihisi nina mwanaume mwingine kwa hiyo amekasirika na kuondoka zake,” mama Shua alijibu huku dhamira ikimuuma kwani alikuwa anaujua ukweli wote…
“Isijekuwa yule kijana mmoja anayekupakupa lifti mama Shua?” aliuliza jirani mmoja…
“Huohuyo…eti ndiyo bwanaangu…”

“Lakini mama Shua kuna yule mama anayefanya kazi mahakamani, aliwahi kutuambia ameshakuona na huyo kijana kama mara tatu mkiwa mnatokea hotelini. Siku moja akasema amemuona huyohuyo kijana akiwa anatoka ndani kwako.”
“Jamani humu ndani si ndiyo kapanga! Anakaa chumba kile pale. Lakini mimi si bwanaangu,” alijitetea mama Shua.

Mara, Musa akaingia ghafla…
“Wewe mama Shua wewe…usije ukarogwa kunitangazia eti mimi nimesababisha ndoa yako ivunjike,” alibwabwaja Musa na kuwafanya wale majirani kushtuka sana kusikia hivyo.
Mama Shua akapoteza fahamu tena. Kuja kuzinduka, yuko mwenyewe, hata Shua hakuwepo. Alikuwa uani na dada wa kazi.
***
Mama Shua alianza maisha mapya akiwa hana mume. Hakutaka kumwambia mama yake mzazi kijijini na wala baba Shua naye hakuwa na habari ya kuwaambia wakwe zake kwamba, amemmwaga binti yao.

Mama Shua alipungua sana, akapoteza nuru yake ya kawaida. Waliomfahamu walishangaa kumwona alivyo. Kwanza, alikuwa mweusi bila ung’avu. Pili, alionesha dhahiri kwamba amekongoroka vibaya sana.
Kila kukicha, mama Shua alikuwa akimtumia meseji, akimpigia simu baba Shua lakini hakupokelewa wala kujibiwa sms zake.
Ndoa ya mama Shua ikawa imevunjikia hap

, kwani baada ya miezi sita kupita, wazazi wake wakajua kila kitu, naye akakiri lakini aliwaumiza sana wazazi hao.

Mama Shua akawa mwanamke wa leo na huyu, kesho na yule, kama mpira. Heshima yake ilishuka kabisa kwani kuna siku wanaume wawili walipigana baa kwa sababu yake, akapasuliwa kichwani.

Lakini mwisho wa yote, alikwenda kijijini kwao na kuangukia kwa wazazi wake kuhusu matendo yake, wakamsamehe kwa maana ya mzazi ni mzazi, wangefanyaje sasa! Lakini baba Shua alimkosa.

MWISHO.

Comments are closed.