CMC Automobiles Yapiga Jeki Mradi wa Madawati wa Rotary
MRADI wa kutoa madawati kwa shule za umma unaoendeshwa na klabu ya Rotary ya Dar es Salaam taongeza idadi ya madawati yanayotolewa baada ya kupata msaada wa gari jipya aina ya Renault kutoka kampuni ya uuzaji magari ya CMC ya jijini Dar es Salaam ili liuzwe na fedha itakayopatikana kutumika kununulia madawati.
Akizungumza wakati wa kupokea gari hilo, rais wa klabu ya Rotary ya Dar es Salaam Nikko Aggarwal amesema fedha zitakazotokana na mauzo ya gari hilo zitachangika katika mradi mkuu wa klabu hiyo wa kutoa madawati kwa shule ambapo hadi sasa klabu hiyo imeshatoa madawati Zaidi ya 1,600 yenye thamani ya Zaidi ya Tsh milioni 250 na hivyo kuwawezesha Watoto takriban 5,000 wa shule mbalimbali kupata madawati.
Rais huyo ameishukuru kampuni ya CMC kwa mchango wake mkubwa kwa klabu hiyo na kwa wanafunzi kwani itaongeza ukubwa wa mradi huo na kuufanya kutoa madawati mengi Zaidi kwa shule zenye uhitaji. Amesema mbali na madawati hayo Zaidi ya 1,600 ambayo yameshatolewa, madawati mengine 400 yanatengenezwa na yatakabidhiwa kwa shule hitaji hivi karibuni.
Hadi sasa kupitia mradi huo, Rotary imeshatoa msaada wa madawati Zaidi ya 1,600 yenye thamani ya Zaidi ya shilingi milioni 250. Klabu hiyo inatarajia kugawa madawati mengine 400 hivi karibuni.