The House of Favourite Newspapers

Corona Imetibua Uchaguzi Mkuu wa Nchi Nyingi Duniani

0

HALI haijulikani itakuwaje kwa nchi nyingi za Afrika ambazo zinatakiwa kufanya uchaguzi mkuu mwaka huu kama Virusi vya Corona vitaendelea kusambaa kwa kasi kubwa iliyopo. Katika baadhi ya nchi duniani, uchaguzi umeahirishwa.

 

Ulimwengu umeshambuliwa na Virusi vya Corona vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19 na sasa nchi nyingi duniani shughuli za kijamii; uchumi na uhusiano, zimevurugika kabisa. Mfano ni Italia, Mungu tunusuru!

 

Nchi 13 za Afrika mwaka 2020, zina ratiba ya uchaguzi mkuu. Shaka ipo Guinea-Bissau ambayo kalenda yake ya uchaguzi wa wabunge ilikuwa Machi 22, mwaka huu. Tayari uchaguzi umeahirishwa.

Awali, uchaguzi huo ulikuwa ufanyike Januari, mwaka jana.

 

Imependekezwa kuwa, uchaguzi nchini Guinea uahirishwe kwa sababu kipindi hiki cha mlipuko wa Virusi vya Corona, si salama kukusanya wapigakura kwenye foleni ili kupiga kura.

Somalia nayo uchaguzi wa wabunge umepangwa kufanyika leo (Machi 27), wakati kesi za maambukizi ya Corona zimeshaanza kuripotiwa.

 

Baadhi ya wanasiasa wanashauri yafanyike makubaliano ya kisheria kuahirisha uchaguzi huo.

Burundi ambayo inatarajiwa kufanya uchaguzi Mei, mwaka huu, wasiwasi ni mkubwa kama zoezi hilo litafanyika kama Virusi vya Corona vitaendelea kutapakaa.

 

Uchaguzi huo ni muhimu kwani pengine utarejesha hali ya amani baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutogombea tena.

Tangu mwaka 2015 Rais Nkurunziza alipoamua kugombea muhula wa tatu, kulimfanya awe Rais wa vipindi vitatu, hali iliyofanya wapinzani wake wa kisiasa kulalamika na kuleta mgogoro uliosababisha Rais Mstaafu wa Tanzania wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kuchaguliwa kuwa msuluhishi.

 

Kutokana na kukosa maelewano, Mkapa alitangaza kujitoa baada ya kudai kunyimwa ushirikiano na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliomteua.

Wagombea urais wa Burundi kwenye uchaguzi wa Mei mwaka, huu ni Evariste Ndayishimiye wa chama tawala, CNDD-FDD, Agathon Rwasa wa CNL, wakati Dieudonne Nahimana ni mgombea binafsi.

 

Nchi nyingine za Afrika ambazo zina kalenda ya uchaguzi mwaka huu na miezi ya uchaguzi kwenye mabano ni Malawi (Julai), Ethiopia (Agosti), Ivory Coast (Oktoba), Tanzania (Oktoba), Burkina Faso (Novemba), Shelisheli (Novemba), Misri (Novemba) na Ghana (Desemba).

 

Marekani uchaguzi wake wa awali kwa wanaowania kuteuliwa na vyama vyao kuelekea uchaguzi wa urais Novemba 3, mwaka huu, umeshaahirishwa katika majimbo mawili ya Louisiana na Georgia kwa sababu ya Corona.

 

Vyombo vya habari nchini humo vimesema endapo virusi hivyo vitaendelea kusambaa Marekani na idadi ya waathirika ikaongezeka hadi Juni mwaka huu, kuna uwezekano mkubwa nchi hiyo ikaahirisha uchaguzi wake.

 

Uchaguzi wa rais Marekani, hufanyika kila baada ya miaka minne. Kutokana na tatizo la Virusi vya Corona, kama italazimu kuahirisha uchaguzi, itabidi Bunge la Marekani na chemba zote mbili, Seneti na Baraza la Wawakilishi, kufanya mabadiliko ya sheria, yasainiwe na Rais Donald Trump kisha sheria hiyo ithibitishwe na Mahakama Kuu na uchaguzi uahirishwe.

 

Nchi 11 za Asia zina kalenda ya uchaguzi pia mwaka huu. Nchi hizo ni Sri Lanka, Mongolia, Hong Kong, Kyrgyzstan, Myanmar na Singapore. Kila nchi yenye kalenda ya uchaguzi mwaka huu, shaka inayoibuka ni uwezekano wa kufanyika kutokana na Virusi vya Corona.

 

Ulaya kuna nchi 20 zinazotarajia kufanya uchaguzi mkuu. Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Teplice, Jamhuri ya Czech uliokuwa ufanyike kati ya Machi 27 na 28, mwaka huu, kujaza nafasi ya Seneta Jaroslav Kubera aliyefariki dunia, tayari umeahirishwa na tarehe nyingine itapangwa baada ya udhibiti wa Ugonjwa wa COVID-19.

 

Wakati huohuo, Jamhuri ya Czech ina kalenda ya uchaguzi wa seneti na mamlaka za mikoa mwaka huu. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Ufaransa, ulikuwa ufanyike Machi 15 mwaka huu, ukasogezwa kwa wiki moja zaidi, mpaka Machi 22, ukashindwa kufanyika kwa sababu ya Virusi vya Corona. Nchi hiyo inakabiliwa pia na uchaguzi wa seneti wa Septemba, mwaka huu.

 

Taarifa rasmi kutoka Serikali ya Serbia, ilieleza kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, uliokuwa ufanyike Aprili 20, mwaka huu. Sababu ni ileile ya Virusi vya Corona.

Poland walipanga kufanya Uchaguzi wa Rais, Mei 10 mwaka huu, lakini kinachosubiriwa ni tangazo la kuahirisha uchaguzi huo.

 

Tangazo hilo la kuahirisha, linasubiriwa pia nchini Iceland ambako walipanga kumchagua Rais wao Juni, mwaka huu, vilevile Lithunia (Oktoba), Jamhuri ya Georgia (Oktoba), Montenegro (Oktoba), Ureno (Oktoba) Croatia (Desemba), Moldova (Desemba) na Romania (Desemba).

 

Mexico, Canada kwa pamoja kalenda yao ya uchaguzi ni mwaka huu, lakini bahati mbaya Ugonjwa wa COVID-19, unatishia uwezekano wa uchaguzi kufanyika.

 

Swali lililo katika vichwa vya watu duniani. Je, Corona itaisha lini ili watu duniani waendelee na shughuli zao za kiuchumi na kisiasa? Tusubiri huku tukimuomba Mungu atuepushie na balaa hili!

Leave A Reply