Corona Yamtikisa Sarah wa Harmonize

KUSAMBAA kwa Virusi vya Corona duniani kote, vinavyosababisha Ugonjwa wa COVID-19, kumemtikisa mpenzi wa staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, Sarah Michelloti ambaye ni raia wa nchini Italia.

 

Nchi ya Italia inaripotiwa kuwa na vifo vingi zaidi kwa nchi za Bara la Ulaya ambavyo ni zaidi ya 2,000.

Kufuatia hali hiyo, mipaka ya nchi hiyo imefungwa hivyo hakuna mtu kuingia wala kutoka, jambo linalomfanya Sarah wa Harmonize au Harmo kushindwa kurudi nyumbani kwao jijini Milan nchini humo.

 

IJUMAA WIKIENDA linafahamu kuwa, Sarah kwa sasa yupo Bongo na kwa mujibu wa watu wake wa karibu, jambo hilo limekuwa likimtia hofu ingawa haoneshi moja kwa moja kwamba ana wasiwasi.

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ alisema kuwa, kufuatia virusi hivyo kuendelea kusambaa na kuwa janga kubwa nchini Italia, baadhi ya watu wanahisi Sarah anaweza kuwa na hofu ya kupoteza ndugu zake, jambo ambalo haliko hivyo.

 

“Kwa upande wa Sarah, wala hana tatizo lolote kwa kuwa hajapata taarifa zozote juu ya ndugu yake kupata virusi hivyo.

“Ndugu wa Sarah wapo kule, lakini hakuna ambaye amepata tatizo la Corona ndiyo maana unamuona Sarah yupo tu Bongo.

 

“Ili kuonesha hajapata taarifa zozote mbaya, hivi karibuni aliposti video yake akiwa anacheza, watu wakawa wanamuandama kwa maneno kwa kuwa ndugu zake wapo Italia ambako Corona imeshamiri.

“Kiukweli naona ana furaha na anaendelea na maisha yake kwa sababu ndugu zake wapo salama, hawajapata tatizo ambalo lipo dunia nzima, ingawa mwanzoni alikuwa na hofu, lakini mpaka sasa hana ndugu ambaye amepata tatizo.

 

“Ni kweli kwa sasa hawezi kutoka kwenda huko kwa sababu Serikali ya Italia imeshatoa tamko kuwa hakuna mgeni au mtu kutoka nje kuingia nchini humo.

“Hata hivyo, sisi (Konde Music) tupo pamoja na Serikali katika kuelimisha jamii kuhusu namna ya kujikinga na virusi hivyo.

 

“Naamini baada ya muda mchache, hali itakuwa shwari na tutaendelea na shughuli za kulijenga taifa kwa ujumla.

“Kikubwa ni kuwasikiliza viongozi wetu kuanzia Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Afya kwa kuwa wao ndiyo wanaohusika kutupa taarifa zaidi kuhusu ugonjwa na kutuelekeza cha kufanya ili kujikinga na maambukizi,” alisema Beauty.

 

Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, bado idadi ya waliopata virusi hivyo nchini walikuwa ni sita ambao wote wanaendelea vizuri.

Ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi wikiendi iliyopita, zilionesha kuwa zaidi ya watu 9,000 wamefariki dunia na zaidi ya 220,000 wameambukizwa Virusi vya Corona duniani kote.

STORI: NEEMA ADRIAN, DAR

Toa comment