Corona Yawatia Mbaroni Wachungaji Wawili

DUNIA ina mambo! Wakati wananchi wakiwa wametaharuki kutokana na kuenea kwa Virusi vya Corona (COVID-19), video zilizosambaa mitandaoni zikiwaonesha wachungaji wawili; Daudi Mashimo na Moses Ibrahim, wakijinadi kupata dawa ya kutibu virusi hivyo, zimesababisha viongozi hao kutiwa mbaroni.

 

Mchungaji wa Kanisa la Mitume na Manabii Tanzania, Daud Mashimo na Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Neno na Maombi lililopo wilayani Arumeru jijini Arusha, Moses Ibrahimu ‘Nabii Namba Saba’, walikamatwa na vyombo vya dola kwa nyakati tofauti ikiwa ni zaidi ya miezi mitatu imepita tangu virusi hivyo vya Corona kuibuka katika Jiji la Wuhan nchini China.

 

Licha ya kwamba virusi hivyo hadi sasa vimeua watu zaidi ya 11,000 na kuenea kwa watu zaidi ya 276,000 duniani, huku vikiwa havina tiba wala kinga, lakini video za wachungaji hao zinawaonesha wakifafanua dawa walizotengeneza na kudai kuwa zinatibu COVID-19.

 

Mchungaji Mashimo alitiwa mbaroni Machi 20, mwaka huu jijini Dar, wakati Nabii Moses alikamatwa Februari 16, mwaka huu na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tisa huko mkoani Arusha.

 

MCHUNGAJI MASHIMO

Aidha, habari kutoka kwa ndugu wa Mchungaji Mashimo, zilieleza kuwa, alikamatwa Machi 20, mwaka huu na kuswekwa rumande katika Kituo cha Polisi Gogoni, Ubungo jijini Dar kwa tuhuma za kujitangaza kuwa anatoa dawa ya kuponya Corona.

 

“Mashimo yupo rumande kwa sababu alitangaza kuwa ana dawa ya kuponya Corona na hii dawa alianza kuitangaza hata kabla huu ugonjwa haujaingia Tanzania, sasa maagizo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kwamba akamatwe, yametekelezwa,” alisema mtoa habari huyo.

Uchunguzi wetu umebaini kuwa, mchungaji huyo yupo mbaroni kwa kufunguliwa jalada la kesi namba; KMR/PE/32/2020 JALADA LA UCHUNGUZI.

 

Kabla ya Virusi vya Corona kuingia Tanzania, Mchungaji Mashimo alitoa dawa iliyohifadhiwa kwenye vichupa vidogo iliyoandikwa kuwa, inatibu Corona ambapo alitupia video za taarifa hiyo kwenye mitandao ya kijamii na kuzua gumzo.

 

NABII NAMBA SABA

Naye Kiongozi wa Kanisa la Huduma ya Neno na Maombi lililopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Moses Ibrahimu almaarufu Nabii Namba Saba, amelieleza Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuwa, baada ya kuhojiwa kwa saa tisa na Jeshi la Polisi mkoani humo, amepeleka ‘sample’ ya dawa yake katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa ajili ya uchunguzi.

 

Alisema Mungu alimpa ufunuo kuhusu dawa ya kutibu virusi hivyo, ndipo akaona ni vema kutumia kitu chochote ili kutibu COVID-19.

“Nimetengeneza ‘udongo wa maajabu’ ambao nimeuombea. Siyo udongo wa kawaida, kwa sababu ni sawa na Yesu alipokuwa anageuza tope au mate na kuwafumbua macho vipofu.

 

“Kwa hiyo na mimi alinifunulia, lakini sikujua taratibu ndiyo maana nikaingia matatani, ila nashukuru Jeshi la Polisi na vyombo vya dola, wamenipa dhamana na sasa nipo uraiani ila naamini majibu yatakapokuja ndipo nitaruhusiwa kutoa huduma au lah,” alisema Nabii Namba Saba.

 

“Sikujua kama kutakuwa na taharuki, nilitamani niweze kufika, naendelea vizuri, wamenipa dhamana. Niko tayari kukutana nao. Sina nia mbaya, silali bila kuombea Taifa langu,” alisema.

 

Kauli hiyo ya nabii huyo imekuja ikiwa umepita mwezi mmoja baada ya Serikali kusema itamchukulia hatua Nabii Namba Saba iwapo atashindwa kuthibitisha kauli yake kuwa ana uwezo wa kutibu wenye maambukizi ya Virusi vya Corona.

 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile katika ziara yake ya kikazi jijini Arusha, alisema anamtaka nabii huyo athibitishe kauli zake.

 

Taarifa za mtu huyo zilisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ndipo Serikali ikatuma wataalam wake kumsaka na kumhoji kama anavyo vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza.

 

Dk Ndugulile alisema yeyote anayetoa tiba asili na mbadala, lazima asajiliwe na Wizara ya Afya, dawa zake ziwe zimesajiliwa na Wizara hiyo na kusisitiza kuwa nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.

 

WENGINE WAFANYA MAOMBI MAZITO

Aidha, wakati wachungaji hao wakihaha kujinasua mikononi mwa vyombo vya dola baada ya kujitangaza kutibu Corona, nchi nzima jana kumefanyika maombi maalum ya kuombea Taifa ili Mungu atokomeze virusi hivyo nchini.

 

Baadhi ya mapaparazi wetu waliotembelea ibada hizo katika Kanisa la The World of Reconciliation Ministries lililopo Ukonga linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi Nabii, Nicholaus Suguye, Kanisa la Mlima wa Moto chini ya Mchungaji Kiongozi, Dk Getrude Rwakatare, Kiongozi wa Kanisa la Inuka Uangaze, Nabii na Mtume Boniface Mwamposa, Kanisa la Nabii Esther Bukuku na Kanisa la Jerusalem la Nabii James Nyakia lililopo Kitunda walishuhudia viongozi hao wakimuomba Mungu.

 

Katika maombi ya wachungaji hao, yalijikita katika kuliombea Taifa ili kutokomeza virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimethibitika kuwapata Watanzania sita.

STORI: GLADNESS MALLYA, DAR

Toa comment