The House of Favourite Newspapers

Costech Yamwaga Milioni 320 kwa Vijana Wabunifu wa Dijitali

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk. Amos Nungu (wa kwanza kulia), Mkurugenzi wa fedha na Utawala kutoka Atamizi ya Teknohama Dar es salaam (DTBi), Makange Mramba (wa kwanza kushoto), anayefuata ni Kiongozi wa Sekta ya Maendeleo kutoka Ubalozi Denmark, Jema Ngwale wakiwa pamoja na vijana washindi nane wa mawazo bunifu ya kibiashara na kidijitali ambao waliwakabidhiwa mtaji wa Sh milioni 120, awamu ya kwanza Costech kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark waliwapatia washindi wengine mtaji wa sh 16 milioni 205.

  TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH ), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark nchini, imekabidhi mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 320 kwa vijana washindi 24 ambao wameandaa mawazo bunifu ya kibiashara na kidijitali kwa lengo la kujiajiri.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya Costech kupitia Kituo atamizi cha teknohama Dar es Salaam (DTBi) kuandaa programu ya uwezeshaji vijana wabunifu kupitia mfumo wa digitali kwa lengo la kuwapatia mafunzo namna kuandaa mawazo ya kibiashara.

 

Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi mtaji washindi nane wa awamu ya pili ya mashindano hayo jijini Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu alitoa wito kwa vijana kutokata tamaa kwa kuwa serikali inawatafutia fursa za kujikwamua kiuchumi kwa kutumia njia mbalimbali.

Kiongozi wa Sekta ya Maendeleo kutoka Ubalozi Denmark, Jema Ngwale (wa kwanza kushoto) akikabidhi hundi ya Sh milioni 120 kwa vijana washindi nane wa mawazo bunifu ya kibiashara na kidijitali ambao walipatiwa mafunzo ya kuandaa maandiko bunifu ya kibiashara na Costech kwa kupitia Atamizi ya Teknohama Dar es Salaam (DTBi) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Denmark.

Alitoa  wito kwa washindi ambao wamefanikiwa  kupatiwa mitaji hiyo kufanya biashara kwa ari ili waweze kuwaajiri vijana wenzao.

Alisema vijana wanapoona kuna fursa yoyote wasisite kushiriki kwa kuwa penye ushindani ndipo mshindi hupatikana bila upendeleo.

“Lengo letu ni vijana kujiajiri na kutoa ajira kwa wenzetu kama sehemu ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

 

Aidha, Mkurugenzi wa fedha na Utawala kutoka Atamizi ya Teknohama Dar es salaam (DTBi), Makange Mramba alisema katika program hiyo ya kuwapatia mafunzo vijana wabunifu wa vyuo vikuu, awamu ya kwanza ya mashindano hayo washindi 16 walipatiwa mitaji ya sh milioni 205 wakati katika awamu ya pili vijana nane wamepatiwa sh milioni 120.

 

Alisema licha ya washindi hao kupatiwa mitaji kulingana na mawazo yao ya kibiashara, washiriki wengine ambao hawakushinda pia walipatiwa mafunzo ya kuandaa maandiko bunifu ya kibiashara ambapo tangu programu hiyo ianzishwe mwaka jana tayari washiriki zaidi ya 1000 wamepatiwa mafunzo.

 

“Kwa hakika tumevuka hata malengo yetu tuliyojiweka kwa zaidi ya asilimia 130,” alisema.

Naye Meneja Biashara na Maendeleo (DTBi), Gasper Mdee alifafanua kuwa licha ya vijana wachache kupatiwa mitaji  hiyo lakini mafunzo waliyopatiwa washiriki wote yanawawezesha kuandika maandiko bunifu ya kibiashara yenye ushawishi wa kupata mitaji katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

 

Aidha, Kiongozi wa Sekta ya Maendeleo kutoka Ubalozi Denmark, Jema Ngwale alitoa wito kwa taasisi mbalimbali zinatoa fursa kwa vijana, kuwapa kipaumbele vijana wa kike ili waweze kujikwamua kiuchumi.

 

“Pia nawashauri vijana kupanua wigo kwa kubadilishana uzoefu kwa kupitia kwa marafiki ili kukuza wazo lako na kuona namna gani unaweza kuvuka, ili usivuke peke yako,” alisema.

Mmoja wa washindi nane wa mawazo bunifu ya kibiashara, Irene Senare akifafanua kuhusu wazo lake la kutengeneza mifuko mbadala. Costech kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark imewapatia washindi hao mtaji wa sh milioni 120 kwa ajili ya kuanza biashara zao.

Mmoja wa washindi hao Othuman Waziri alisema; “Wazo langu ni kutengeneza Boxpesa ambayo ni progamu maalumu itakayowasaidia Watanzania kutunza fedha zao kwa njia ya mitandao kwa muda maalumu”.

 

Wakati Irene Sinare alisema wazo lake kutengeneza mifuko maalumu mbadala ambayo ina uwezo wa kupotea kwenye udongo ndani ya siku 180.

 

“Mifuko hii imetengenezwa kwa malighafi ambayo ni rafiki wa mazingira, na imekuja wakati maufaka ambao serikali imepiga marukufu matumizi ya mifuko ya plastiki kwani inachukua miaka 500 kupotea kwenye udongo,” alisema.

NA MWANDISHI WETU

Comments are closed.